Coastal yaanza na ukuta chuma

MABOSI wa Coastal Union wanaendelea kufanyia maboresho kikosi ambapo kwa sasa wako katika mazungumzo kumsajili beki wa Mbuni inayoshiriki Ligi ya Championship, Ambokise Mwaipopo.

Nyota huyo anayecheza beki wa kati alijiunga na Mbuni dirisha kubwa lililopita baada ya KenGold ya Mbeya aliyoichezea kushuka Ligi Kuu.

Taarifa kutoka Coastal Union zimedai Mwaipopo alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Mbuni japo unaomruhusu kujiunga na timu yoyote itakayomtaka katika dirisha dogo, jambo linalowaingiza vitani ‘Wagosi wa Kaya’ kumtaka.

Mbali na Ambokise, Coastal Union inafuatilia saini ya aliyekuwa beki wa kulia wa Geita Gold, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji na JKT Tanzania, George Aman Wawa ili kwenda kuongezea nguvu katika kikosi hicho.

Mwanaspoti linatambua Wawa ni pendekezo la Kocha Mohamed Muya, ambapo mazungumzo kati ya pande hizo  mbili yanaendelea.

Coastal inapambana kuboresha kikosi ambacho kimeachana na kipa Fales Gama pamoja na kiungo Khleffin Hamdoun, ambaye tayari ameshakamilisha usajili wa kujiunga na Dodoma Jiji.

Coastal itashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 usiku, Januari 18, 2026 kuvaana na Azam FC katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara iliyorejea jana.