Wananchi Siha waiomba Serikali kuharakisha usajili Sekondari Mondo Memusi

Siha. Wananchi wa Kijiji cha Donyomurwak wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuharakisha usajili wa Shule mpya ya Sekondari Mondo Memusi ili ianze kutoa huduma za elimu kikamilifu.

Ombi hilo limetolewa leo Januari 17, 2026, katika hafla fupi iliyofanyika Kijiji cha Oloiwang, wakati Shirika la Mondo UK kwa kushirikiana na Mondo Tanzania walipokabidhi rasmi shule hiyo kwa Serikali baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.

Wananchi wamesema ujenzi wa shule hiyo umeondoa changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi waliolazimika kutembea umbali wa kilometa 24 kila siku kwenda na kurudi kusoma katika Shule ya Sekondari Sekirari. Kwa sasa, wamesema ndoto ya watoto wao kupata elimu karibu na makazi yao imetimia.

Wakizungumza baada ya hafla ya makabidhiano, wananchi wamesema kilichosalia ni Serikali kuharakisha usajili wa shule hiyo ili ianze kupokea wanafunzi mapema.

“Ni kweli, ombi letu la kwanza ni Serikali kusaidia kuharakisha usajili wa Shule ya Sekondari Mondo Memusi, ambayo inahudumia zaidi jamii ya wafugaji, ili ianze kufanya kazi kikamilifu kwa manufaa ya watoto wetu,” amesema mwananchi mmoja.

Mkazi wa eneo hilo, Paulina Israel amesema hapo awali watoto walikuwa wakiamka saa kumi usiku kujiandaa kwenda shule kutokana na umbali mrefu, hali iliyosababisha uchovu, kuchelewa masomo na changamoto nyingine za kijamii, ikiwemo baadhi ya watoto wa kike kupata ujauzito wakiwa njiani au shuleni.

Kutokana na changamoto hizo, alisema wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao walianzisha ujenzi wa shule hiyo hadi hatua ya msingi, kabla ya Shirika la Mondo UK na Mondo Tanzania kuunga mkono juhudi hizo kwa kujenga vyumba vinne vya madarasa, ofisi mbili za walimu, matundu 12 ya vyoo kwa wanafunzi pamoja na meza na viti 100.

“Ujenzi umekamilika; kinachosalia sasa ni usajili. Tunaiomba Serikali ichukue hatua za haraka ili watoto waanze masomo,” amesema Paulina.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka amewahakikishia wananchi kuwa usajili wa shule hiyo utafanyika ndani ya mwezi huu wa Januari 2026, ili kuwezesha wanafunzi kuhamishwa kutoka Shule ya Sekondari Sekirari.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Siha, Alfred Mosi, ameyapongeza mashirika hayo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya elimu.

Awali, mdau wa maendeleo wa wilaya hiyo, Mwalimu Meijo Laizer, alisema gharama ya jumla ya miradi ya elimu katika vijiji vya Donyomurwak na Oloiwang ni zaidi ya Sh200 milioni, ikilenga kuboresha upatikanaji wa elimu na kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.