Dodoma. Wakurugenzi wa halmashauri nchini Tanzania wameagizwa kusimamia na kuwa mfano wa kupunguza matumizi ya plastiki katika ofisi zao ili kulinda mazingira.
Agizo hilo limetolewa leo Januari 17, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Profesa Peter Msofe wakati akizindua mradi wa urejeshaji wa mazingira na uoto wa asili.
Mradi huo wa miaka mitano unasimamia na World Wildlife Fund (WWF) na kutekelezwa katika Wilaya za Mpwapwa na Chamwino (Dodoma) na Korogwe na Kilindi (Tanga).
Profesa Msofe amesema ni aibu wakurugenzi kuwa waangalizi kwenye uharibifu wa mazingira na hawatakiwi kuwa wapanga kazi badala yake wawe wasimamizi wa kazi hizo wakianzia wao kuonyesha mfano.
“Katika hili sitaki mkafanye, bali naagiza lazima litekelezwe tena iwe nchini nzima, na mshirikishe walio chini yenu na jamii inayowazunguka, lazima mtambue kwenye mazingira tuna hali mbaya na hivyo hatuwezi kucheka,” amesema Profesa Msofe.
Kuhusu mradi huo amesema ni lazima uwe wa kiushindani katika mpango wa urejeshaji wa uoto wa asili ambapo Tanzania imejenga kufikia hekta milioni 5.2 wakati bara la Afrika ni hekta milioni 100 na kwa upande wa Dunia zinatakiwa kufikia hekta milioni 350 ifikapo 2050.
Ofisa kutoka WWF Almas Kashindye ametaja lengo katika mradi huo ni kuboresha maisha ya wananchi na kulinda bayonuwai.
Kashindye amesema mradi huo unagharimu Sh5.4 bilioni huku walengwa zaidi wakiwa watu wa vijijini katika wilaya zilizoonekana kuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Msimamizi wa mradi huo uliopewa jina la IKI Forest Landscape, Raymond Kallenga amesema mbali na Tanzania mpango huo unatekelezwa kwa nchi za Uganda, Madagasca, Brazil, Peru na Colombia na mfadhiri ni Ujerumani.
Killenga anasema mkakati waliouweka ni ufuatiliaji zaidi katika kila hatua ili kuhakikisha wanapata matokeo kama ilivyo.