Bwana Yesu asifiwe, karibu kwenye somo la leo Jumapili lenye kichwa kinachosema ‘Usiwe kama wale wakoma tisa’.
Msingi wa somo letu linapatikana: Luka 17:11–19 “Je, wale waliotakaswa hawakuwa kumi? Wako wapi wale tisa? Hakupatikana mtu aliyerudi kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” (Luka 17:17–18)
Yesu alipokuwa akisafiri kuelekea Yerusalemu, alikutana na wanaume kumi waliokuwa na ugonjwa wa ukoma.
Ugonjwa huu uliwatenga na jamii, familia, na ibada. Kwa sauti kubwa walipaza sauti wakisema, “Yesu, Mwalimu, uturehemu.” Yesu aliwasikia, akawaponya wote kumi. Lakini Biblia inatuambia kwamba ni mmoja tu aliyerudi kumshukuru Mungu.
Wale wengine tisa walipokea muujiza, lakini hawakurudi kutoa shukrani.
Leo, somo hili linatuuliza swali muhimu, je, sisi ni kama yule mmoja aliyerudi, au kama wale wakoma tisa waliokwenda zao bila shukrani?
Wote walipokea baraka, lakini siyo wote walishukuru
Yesu hakumponya mmoja tu, aliwaponya wote kumi. Hii inatuonyesha kuwa Mungu ni mwema na hutoa baraka hata kwa wale wasiomshukuru. Katika jamii yetu leo, watu wengi wamepokea baraka nyingi: afya njema, kazi, biashara, elimu, familia, na ulinzi wa Mungu. Lakini ni wangapi wanaokumbuka kurudi kumshukuru Mungu?
Mfano mtu anapopata kazi baada ya maombi ya muda mrefu kwa Mungu. Anapokuwa hana kazi, kanisani yupo kila ibada, anaomba msaada wa maombi. Lakini akishapata kazi, anapotea kanisani, hana tena muda wa Mungu. Huyu anafanana sana na wale wakoma tisa.
Biblia inatukumbusha, “Shukuruni kwa kila jambo.” (1 Wathesalonike 5:18)
Kutokushukuru ni dalili ya moyo usiojali
Wale wakoma tisa hawakuwa watu wabaya, lakini walikuwa na mioyo isiyojali. Waliona muujiza kama kitu cha kawaida. Pia jamii yetu imezoea baraka kiasi kwamba hatuzioni tena kama neema ya Mungu.
Tunapopumua bila mashine, tunatembea, tunaona, tunakula haya yote ni baraka. Lakini mara nyingi tunaanza kumkumbuka Mungu pale tu tatizo linapokuja. Mtu anaweza kulalamika kwa Mungu kwa kukosa kitu kimoja, huku akipuuza baraka kumi alizonazo.
Mithali 15:13; inasema:“Moyo wenye furaha huufanya uso kung’aa.”
Moyo wa shukrani huleta furaha, lakini moyo wa kukosa shukrani huleta manung’uniko.
Yule mmoja aliyerudi alipokea zaidi ya uponyaji
Yesu alipomwona yule mmoja aliyerudi, alimwambia:“Imani yako imekuponya.” (Luka 17:19)
Hapa tunaona kuwa yule mmoja hakupata uponyaji wa mwili tu, bali pia wokovu wa roho. Shukrani ilimfungulia mlango wa baraka kubwa zaidi. Hii inatufundisha kuwa shukrani humweka mtu karibu zaidi na Mungu.
Katika jamii, mtu anayejua kushukuru hupendwa, huaminiwa na husaidiwa zaidi. Vivyo hivyo katika mambo ya kiroho, Mungu hupendezwa na moyo wa shukrani.
Zaburi 50:23 inasema:“Atayetoa sadaka ya shukrani hunisifu.”
Usiwe kama wale wakoma tisa
Mahubiri haya yanatukumbusha tusifanye kosa la wale wakoma tisa. Tusipokee baraka na kusahau chanzo chake. Tusiponywe na Mungu halafu tuendelee kuishi kana kwamba hatumjui.
Katika familia, ni vyema watoto kuwashukuru wazazi wao. Katika jamii, ni vyema kuwashukuru wanaotusaidia. Na zaidi ya yote, ni wajibu wetu kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Kila unapopata mshahara, unapopona ugonjwa, unapofanikisha jambo, au unapopitia hatari na kuokoka rudi kwa Mungu na sema asante.
Tusikubali MUNGU atushangae na kutulaumu kama alivyoshangaa Bwana Yesu kwa kitendo cha kukosa shukrani wakoma kenda kati ya kumi walioponywa!
Kuna kujisahau kwa haraka hasa pale tunapokuwa na afya njema.
Wakoma walipokuwa na ugonjwa ule mbaya walikuwa wanatafuta msaada wa uponyaji kila mahali waliposikia wanaweza kupata uponyaji.
Lakini walipoponywa na Bwana Yesu, hawakuona sababu ya kulipa gharama ya kurudi kushukuru isipokuwa mmoja tu kati yao.
Hali ya kukosa shukrani inamshangaza Mungu, inamvunja moyo Mungu, inazuia baraka na miujiza ya baada ya shukrani.
Ni vema kujua kuwa, Mungu ametutendea mema mwaka mzima 2025 na sasa tumeanza Januari tukiwa na afya njema, familia zina afya njema, wazazi wana afya njema, wamefanikiwa katika kazi na biashara zao.
Wamekuwa na mafanikio ya kielimu, wamekuwa na amani, wamefanikisha mambo ya ujenzi, ununuzi wa vitu mbalimbali.
Pia Mungu amezuia matukio ya huzuni ya ajali, ulemavu, vifo nk.
Kwa sababu ya wema wote wa Mungu, jipange kurudi madhabahuni kumpa Mungu utukufu kwa dhabihu ya shukrani ya wema na fadhili zake za mwaka mzima unaonza.
Leo, Yesu bado anauliza swali lilelile: “Wako wapi wale tisa?” Swali hili linatuhusu sisi. Je, sisi ni watu wa kulalamika au watu wa kushukuru? Je, tunaomba tu wakati wa shida, au tunamshukuru Mungu hata wakati wa neema?
Chagua kuwa kama yule mmoja aliyerudi. Chagua moyo wa shukrani. Usiwe kama wale wakoma tisa.
Mchungaji Dickson Keneth anapatikana Kilombero, Morogoro