Mapya yaibuka aliyeua watoto watatu wa familia moja

Mbeya. Siku moja baada ya Polisi Mkoa wa Mbeya kueleza kuwa wanamshikilia Dotto Lubogeja (22) kwa tuhuma za kuwaua watoto watatu wa familia moja, taarifa mpya kuhusu tukio hilo zimeibuka, ikiwemo simulizi ya jinsi mtuhumiwa huyo alivyoawa na wananchi.

Jeshi la Polisi, kupitia taarifa yake, lilisema mtuhumiwa huyo aliwanyonga watoto hao watatu ambao ni Petro Amos (8), Sam Amos (6) na Nkamba Amos (4), wote wa familia moja katika Kijiji cha Matundasi, Wilaya ya Chunya, baada ya kuwakuta wakichunga ng’ombe katika mlima jirani na nyumbani kwao.

Taarifa ya Polisi ilieleza kuwa baada ya kuwaua, mtuhumiwa alitupa miili ya watoto hao katika korongo lililopo umbali wa kilometa 22 hadi 25, katika Kitongoji cha Mwashota, Kata ya Madundasi, wilayani humo.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana Ijumaa, Januari 16, 2026 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa, ilisema tukio hilo lilitokea Januari 15, 2026 katika Kijiji cha Matundasi na kwamba baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa aliiba ng’ombe 15 waliokuwa wakichungwa na watoto hao.

Kaimu Kamanda huyo alisema mtuhumiwa alifanikiwa kuuza mifugo hiyo kwa thamani ya Sh5.1 milioni. Aliongeza kuwa Polisi walianza msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo pamoja na mjomba wake, anayedaiwa kuhusika kuficha ng’ombe hao.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali, hali iliyosababisha kukatishwa uhai wa watoto wasio na hatia.

Wakati Polisi wakieleza hayo jana Januari 16, 2026, leo Jumamosi, Januari 17, 2026, viongozi mbalimbali wa eneo hilo wameeleza tukio lilivyotokea hadi wananchi walivyomshambulia mtuhumiwa huyo na kusababisha kupoteza maisha yake mbele ya Polisi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Madundasi, Ismail Kassim, amesema mauaji ya watoto yalitokea kwa nyakati tofauti Januari 12 na 13, wakati baba wa watoto hao, Amos Simkamba (55), akiwa amesafiri kumtafuta mkewe aliyetoroka.

Amesema mtuhumiwa baada ya kuiba ng’ombe hao 15, aliwaua watoto wawili wadogo, kisha akaenda kusaka wateja akiambatana na yule mkubwa, Petro Amos (8), kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa soko.

Baada ya kufanikisha kuuza ng’ombe hao kwa Sh5.1 milioni, alirejea katika mlima alipowakuta awali, ambapo pia alimuua kwa kumnyonga mtoto wa tatu na kumtupa korongoni.

Kassim amesema mtuhumiwa kisha alimpigia simu baba wa watoto hao, Amos Simkamba (55), akamtaka arejee nyumbani akidai yeye anajua aliko mkewe.

“Mbali na hilo, pia alielezwa kuhusu kuwepo biashara ya ng’ombe zake, jambo ambalo lilimshtua Simkamba na kulazimika kumpigia simu Mtendaji wa Kijiji juu ya tukio hilo, ndipo uongozi ukaanza ufuatiliaji,” amesema.

Amesema baada ya taarifa hizo, walianza kumsaka Lubogeja kwa kushirikiana na mgambo na kufanikiwa kumkamata. Baada ya kumuhoji, alitoa ushirikiano mkubwa na kuonyesha eneo alipouza mifugo na sehemu alipohifadhi Sh5.1 milioni alizopata baada ya kuuza.

Amesema baada ya kumhoji zaidi ndipo aliwapeleka kwenye korongo ilipokuwa miili ya watoto hao na kukiri aliwaua kwa kuwanyonga shingo wawili Januari 12 na mwingine Januari 13.

“Baada ya kutoa ushirikiano huo, tulitoa taarifa Kituo cha Polisi na askari walifika mpaka eneo la tukio na kuchukua miili ya watoto hao kwa taratibu nyingine na kukabidhi kwa ajili ya mazishi, kisha kumkamata mtuhumiwa,” amesema Kassim.

Amesema baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kukiri kufanya mauaji hayo, hali ilikuwa mbaya kwani wananchi walitaka kuvunja Ofisi ya Mtendaji, nao walilazimika kuomba msaada kwa Polisi, ambao walifika na kuwatawanya wananchi.

“Kimsingi tunalipongeza Jeshi la Polisi; walifika kwa wakati kutuliza wananchi, lakini kutokana na jamii kuwa na hasira kwa kuchoshwa na matukio ya mauaji katika kitongoji hicho, waliwazidi nguvu Polisi na kumvuta mtuhumiwa na kumshambulia kwa kipigo,” amedai.

Mtendaji huyo amesema walimchukua mtuhumiwa na kumpeleka Kituo cha Afya Utengule wilayani humo na baadaye walipigiwa simu wakitakiwa kuieleza familia ya mtuhumiwa kwamba amefariki dunia na mwili wake umehifadhiwa kwenye kituo hicho cha afya.

“Baada ya kupigiwa simu, nilimpigia simu Mwenyekiti wa Kitongoji ambaye aliijulisha familia hiyo na mazishi yake yanafanyika leo Januari 17, 2026,” amesema Kassim.

Mwananchi limemtafuta Kaimu Kamanda Siwa ili afafanue mabadiliko ya taarifa hizo bila mafanikio.

Aidha, si Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Maulid Surumbu, wala Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, aliyepatikana kwa kuwa simu zao ziliita bila kupokewa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Madundasi, Ben Mbegeni, amesema watoto hao waliouawa walikuwa wakiishi peke yao baada ya baba yao kuondoka kwa madai ya kumtafuta mkewe aliyekimbia na kaka yao waliyeachiwa kuondoka.

Amesema Januari 6 mwaka huu baba mzazi wa watoto hao aliomba barua ya Serikali ya Mtaa kwa ajili ya kwenda kumtafuta mke wake Wilaya ya Chunya, ambako alipata taarifa ndiko alipokimbilia.

Mwenyekiti huyo amesema kutokana na kukosa usimamizi na usaidizi wa karibu, watoto hao walikosa haki ya kupata elimu na badala yake walijikita katika kuchunga ng’ombe.

Amesema kitongoji walichokuwa wakiishi ni mbali na kimejitenga sana, namna ya kuwafikia ni vigumu, na kimekuwa na matukio mengi ya kihalifu hususan mauaji.

Kiongozi huyo amesema hilo ni tukio la tatu la mauaji, hivyo ameiomba Serikali kukifuta kutokana na kufululiza kwa matukio hayo.

“Hicho kitongoji ni kama hakina Serikali; watu wake wanafanya matukio mabaya na hata mauaji kutokana na kuwepo maeneo ya hifadhi ambapo hata likitokea tukio, ufikaji wake ni mgumu kutokana na jiografia yake,” amesema Mbegeni.

Alipotafutwa kwa njia ya simu na Mwananchi, baba mzazi wa watoto hao, Amos Simkamba (55), amesema kwa sasa hawezi kuongea chochote kutokana na maumivu aliyonayo na mazingira ya safari aliyonayo.

“Naomba mniache kwanza, sitaki kuongea chochote; nina maumivu makali ya wanangu watatu kuuawa bila hatia, niko safarini pia,” amesema.

Kwa upande mwingine, kaka wa mtuhumiwa aliyeuawa, Mami Kurwa, amesema anashangazwa kusikia taarifa za kuuawa kwa mdogo wake wakati jana Januari 16, 2026 alielezwa kuwa anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji.

“Marehemu ni mdogo wangu; tuko mama mmoja baba tofauti na tunaishi vitongoji tofauti. Yeye anaishi Lyanjunga na mimi naishi Masenjele, lakini leo napata taarifa tofauti baada ya kupigiwa simu kuwa aliawa kwa kipigo,” amesema.

Amesema marehemu mdogo wake ameacha mke na mtoto mmoja na changamoto iliyopo ni jiografia ya maeneo yao pamoja na mtandao wa simu kuwa hafifu, hivyo taarifa nyingine kuhusu msiba hakuwa nazo.