Songea. Ikiwa ni mwezi mmoja na siku sita tangu aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama afariki dunia, Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea kimetangaza mchakato wa ndani wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.
Mhagama ambaye alikuwa waziri katika Serikali za awamu tofauti, alifariki dunia Desemba 11, 2025, hivyo kuacha wazi nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwa umma na Katibu wa CCM Wilaya ya Songea, Juma Nambaila leo Januari 18, 2026, wanachama wenye sifa wametakiwa kujitokeza kutia nia ya kugombea nafasi hiyo ya ubunge.
Amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu utaanza leo Januari 18, 2026 na utafungwa siku inayofuata, Januari 19, 2026 na muda wa kuchukua fomu ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Aidha, ametoa wito kwa wanachama wote wenye sifa na nia ya kugombea kuzingatia maelekezo ya CCM pamoja na kuhakikisha kuwa fomu zinarejeshwa ndani ya muda uliopangwa, huku zitakazorejeshwa nje ya muda hazitapokelewa.