Mbeya. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya imeanza mchakato wa ujenzi wa barabara mpya ya mchepuko katika eneo la Mlima Nyoka ili kukabiliana na msongamano wa malori katika Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam).
Barabara hiyo itakuwa na urefu wa kilometa 48.9 na itajengwa kwa kiwango cha lami, ikipita nje ya Jiji la Mbeya hadi mkoani Songwe. Mradi huo unalenga kutoa suluhu ya kudumu ya foleni ndefu, ajali za mara kwa mara na vitendo vya wizi wa mizigo ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika eneo hilo lenye mwinuko mkali.
Akizungumza Januari 16, 2026, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Suleiman Bishanga amesema ujenzi wa barabara ya mchepuko ni mkakati wa kupunguza adha kwa madereva wa masafa marefu wanaotumia njia hiyo muhimu ya kibiashara inayounganisha Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na SADC.
Amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati, Tanroads imewashirikisha wazee wa mila kutokana na historia na imani za jadi zinazohusishwa na eneo la Mlima Nyoka, hatua iliyosaidia kupata ridhaa na baraka za viongozi wa kimila.
“Tunashukuru wazee wa mila kwa kuubariki mradi huu ambao una faida kubwa kwa uchumi wa taifa na usalama wa wasafirishaji,” amesema Bishanga.
Kiongozi wa Mila Jiji la Mbeya na Mbeya Viijijini, Chifu Rocket Mwanshinga akitoa maelekezo ya maeneo ya matambiko katika mlima nyoka kwa watendaji wa Tanroad baada ya kutembelea eneo ambalo wanajenga barabara ya mchepuko yenya urefu wa kilometa 48.9. Picha na Hawa Mathias
Ameongeza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi huo ikitambua umuhimu wake katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na kupunguza changamoto ya magari kukwama barabarani.
Katika kulinda rasilimali za asili, Bishanga amesema Tanroads itahakikisha maelekezo ya viongozi wa mila yanazingatiwa, hususan katika uhifadhi wa miti na misitu ya asili itakayopitiwa na mradi huo.
Kuhusu udhibiti wa uhalifu, amesema Tanroads kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) wameweka mikakati madhubuti ya kudhibiti wizi wa mizigo, hasa nyakati za jioni kunapokuwa na msongamano mkubwa wa magari.
Meneja wa Miradi ya Barabara Kuu Tanroads, Chama Wambura amesema Mlima Nyoka ni eneo lenye mwinuko mkali unaosababisha ajali, vifo na uharibifu wa mali kutokana na mzigo mkubwa unaobebwa na barabara hiyo.
Alisema ujenzi wa barabara ya mchepuko utasaidia kutoa maeneo ya magari kupumzikia na kupunguza hatari kwa madereva wanaopanda mlima huo maarufu kwa changamoto zake.
Akizungumzia imani za jadi, Kiongozi wa Machifu wa Jiji la Mbeya na Wilaya ya Mbeya Vijijini, Chifu Rocket Mwashinga, amesema Mlima Nyoka ni eneo la kihistoria na kimila, akieleza kuwa viongozi wa mila wamefanya maombi maalumu ili kuubariki mradi huo kabla ya kuanza ujenzi.
Amesema viongozi wa mila wanaunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mbeya.
Kwa upande wa madereva, dereva wa masafa marefu kutoka Malawi, Ally Mbaula, amesema ujenzi wa barabara hiyo utapunguza muda wa safari na kuwasaidia madereva kufanya kazi zao kwa usalama na ufanisi zaidi.