Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, kufuatia kifo cha mbunge wa viti maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kundi la wafanyakazi, Halima Idd Nassor.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 18, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia ameeleza kuwa marehemu alikuwa kiongozi mahiri na mwenye mchango mkubwa kwa chama na Taifa kwa ujumla, hususan katika kutetea masilahi ya wafanyakazi na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia majukumu yake ya kibunge na ndani ya CCM.
Pia, Rais Samia ametoa pole kwa familia ya marehemu, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wanachama wote wa CCM, wabunge pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo mzito.
“Nawaombea wafiwa subira, faraja na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi, huku tukimuomba Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda amesema kifo cha Halima ni pigo kwa jumuiya hiyo kutokana na mchango wake katika chama na jamii kwa ujumla.
Chatanda amesema marehemu alikuwa mchapakazi, mzalendo na mwenye mapenzi makubwa kwa chama chake hususan jumuiya ya UWT.
“Kwa kweli tumeondokewa na mtu aliyekuwa anajituma sana katika utendaji wa kazi za chama na jumuiya. Alikuwa ni mtu tuliyekuwa tunamtumainia, lakini tunamshukuru Mungu kwa yote,” amesema Chatanda.
Kwa mujibu wa Chatanda ambaye pia ni mbunge, marehemu Halima alihudhuria kikao cha kwanza baada ya kuahirishwa, hata hivyo baadaye alianza kuugua kutokana na tatizo la moyo na kulazwa hospitalini.
“Jana, nilienda kumuona hospitalini na hali yake ilikuwa inaendelea vizuri na alionyesha matumaini, lakini asubuhi nimepigiwa simu nikaarifiwa kuwa amefariki dunia, jambo lililonishangaza sana,” amesema.
Amesema marehemu ameondoka akiwa ameacha matumaini makubwa kwa wananchi, hususan wanawake waliomchagua, akiahidi kuwahudumia na kuhakikisha wanapata maendeleo ya kiuchumi.
Akielezea historia yake kwa ufupi, Chatanda amesema marehemu Halima alikuwa mtumishi wa umma katika idara ya ardhi na baada ya kutangazwa kwa nafasi za uongozi aligombea ndani ya UWT kupitia kundi la wafanyakazi Tanzania Bara.
“Mungu alimjalia akashinda na baadaye akawa Mbunge wa Viti Maalumu,” amesema.
Mbunge wa Kigamboni, Allan Sanga amesema kifo cha Halima kimeacha mshtuko mkubwa kutokana na mipango na matarajio makubwa aliyokuwa nayo ya kuwatumikia wananchi wa Kigamboni kutatua changamoto zinazomkabili.
Sanga amesema alikutana na marehemu kwa muda mfupi wakati wa kikao cha ufunguzi wa Bunge na hafla ya kuapishwa, ambapo alimfuata na kujitambulisha kuwa ni mwananchi wa Kigamboni anayeishi Kibada na kumuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi.
Amesema aliipokea ahadi hiyo kama chachu ya maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano wa viongozi na wanachama wengi unaongeza nguvu katika kusukuma mbele ajenda za wananchi na kuharakisha utekelezaji wa maendeleo.
“Kifo chake kimenishtua kwa sababu alikuwa dada anayejua anachokitaka na alikuwa na malengo makubwa. Nilikuwa na matarajio ya kufanya kazi naye kwa pamoja kuwatumikia wananchi wa Kigamboni,” amesema Sanga.
Ameongeza kuwa dhamira yake ilikuwa ni kushirikiana kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi, lakini amekiri kuwa mapenzi ya Mungu yametangulia.
Sanga amebainisha kuwa marehemu alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na mtumishi wa umma, ingawa hakuwahi kufanya kazi naye moja kwa moja.
Amesema marehemu alikuwa mkazi wa Kibada na wazazi wake wanaishi eneo hilo, huku taratibu za mazishi zikitarajiwa kufanyika leo jioni.
Sanga amesema hatoweza kuhudhuria msiba huo kwa kuwa yuko nje ya mkoa, ingawa atatuma wawakilishi katika msiba huo.
Awali taarifa iliyotolewa na Bunge ilieleza kuwa mazishi ya mbunge huyo yatafanyika leo Jumapili, Januari 18,2025 kwenye makaburi ya Kibada kwa Dole, Kigamboni jijini Dar es Salaam.