SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAMALIZA KERO YA MAFURIKO KAHE, WANANCHI WASHUKURU

:::::::::

 Wananchi wa eneo la Kahe, Wilaya ya Moshi Vijijini, wameeleza furaha na shukrani zao baada ya changamoto ya muda mrefu ya mafuriko yaliyokuwa yakisababishwa na Mto Dehu kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia zoezi la kudabua mto huo.

Kwa zaidi ya miaka minane, Mto Dehu ulikuwa ukifurika mara kwa mara na kusababisha uharibifu mkubwa wa mashamba, makazi na miundombinu ya kijamii, hali iliyowaathiri kiuchumi na kijamii wananchi wa maeneo ya jirani.

Hatua ya kudhibiti mto huo imetokana na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mheshimiwa Enock Zadock Koola, kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo kufanikisha upatikanaji wa vifaa maalumu vya kudabua mto huo.

Wananchi wa Kahe wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio chao na kukipatia ufumbuzi wa kudumu, wakisema hatua hiyo imerejesha matumaini ya maisha salama na yenye tija.

Pongezi pia zimetolewa kwa Mbunge Koola pamoja na Diwani wa Kata ya Kahe Magharibi, Abdul Msangi, kwa ufuatiliaji wa karibu, uharakishaji na kusimamia utekelezaji wa mradi huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu bila mafanikio.

Ikumbukwe kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mbunge Koola aliwasilisha moja kwa moja kilio cha wananchi wa Kahe mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alitoa ahadi ya kupatikana kwa suluhu ya haraka.

Wananchi pamoja na viongozi wa eneo hilo wamesema utekelezaji wa zoezi la kudabua Mto Dehu umeimarisha usalama wa makazi, kurejesha tija ya shughuli za kilimo na kuweka msingi wa maendeleo endelevu katika eneo la Kahe.