Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka India, inatarajia kuanza kufanya upasuaji wa kisasa wa kutibu tezi dume kwa kutumia teknolojia mpya ijulikanayo kitaalamu kama Rezum Water Vapor Therapy, ambao utafanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Teknolojia hiyo hutumia mvuke wa maji na huchukua takribani dakika 15 hadi 20 kukamilika, tofauti na upasuaji wa awali uliokuwa ukichukua hadi saa moja. Njia hiyo mpya inatarajiwa kutoa suluhu kwa wagonjwa wengi zaidi wanaosumbuliwa na tatizo la tezi dume pamoja na kuboresha kwa ujumla huduma za afya nchini.
Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo kwa wanaume (Urolojia) wa Hospitali ya KCMC, Dk Frank Bright, amesema hospitali hiyo itaendesha kambi ya siku sita kuanzia Januari 26 hadi 31, ambapo wagonjwa watapata fursa ya kufanyiwa upasuaji huo na kuruhusiwa ndani ya siku moja.
“Tunaleta huduma ya Rezum Water Vapor Therapy inayotibu tezi dume iliyovimba kwa muda mfupi sana. Ndani ya dakika 15 hadi 20 mgonjwa anakuwa ameshapatiwa matibabu, tofauti na njia za awali zilizokuwa zinachukua saa moja,” amesema Dk Bright.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo ina madhara madogo ukilinganisha na upasuaji wa kawaida, kwani hutumia muda mfupi na haina upotevu mkubwa wa damu kutokana na matumizi ya mvuke wa maji.
Kwa mujibu wa Dk Bright, awali hospitali ilikuwa ikifanya upasuaji wa tezi dume kwa wagonjwa kati ya 400 hadi 600 kwa mwaka, lakini kwa kutumia teknolojia hiyo mpya idadi ya wagonjwa watakaohudumiwa itaongezeka kwa kiasi kikubwa. Pia, badala ya kufanyiwa upasuaji wagonjwa sita hadi 10 kwa siku, sasa hospitali itaweza kuhudumia hadi wagonjwa 20 kwa siku.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo, amesema, “Tuliona ni vyema kuwaleta wataalamu hapa nchini ili kupunguza gharama kwa wagonjwa wetu, kwani si kila Mtanzania ana uwezo wa kugharamia matibabu nje ya nchi,” amesema Chisseo.
Ameongeza kuwa hospitali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu, ajira na mafunzo ya wataalamu wa afya ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Tanlink, Baraka Farles, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiratibu kambi mbalimbali za matibabu kwa kushirikiana na madaktari kutoka India kama sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya nchini.