SERIKALI YAIMARISHA MKAKATI WA UJENZI WA BARABARA ZA HARAKA KUPITIA UBIA (PPP)

……..

Serikali imeendelea kuimarisha maandalizi ya ujenzi wa miradi ya barabara za haraka (Expressways) kupitia mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), ikiwa ni mkakati wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu nchini.

Hatua hiyo imebainishwa Januari 17, 2026, jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameongoza kikao cha kazi kilicholenga kutathmini na kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Aidha kikao hicho kimewakutanisha viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi; Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega; pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. James Kilabuko; Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara; na watendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, David Kafulila.