Chelsea Ngole ataja ugumu WPL

MECHI sita alizocheza golikipa wa Tausi FC, Chelsea Ngole zimemuamsha kupambana zaidi kuhakikisha anaisaidia timu hiyo kutoruhusu bao.

Chelsea alijiunga na Tausi msimu huu akitokea Louves Minproff FC ya Cameroon alikokuwa kipa namba moja wa timu hiyo.

Akizungumzia mechi sita alizocheza Chelsea amesema mechi ngumu zaidi ilikuwa dhidi ya Simba Queens waliyopoteza mabao 3-0 akitaja kutokuwa na mawasiliano ni miongoni mwa mambo yaliyowaangusha.

Kipa huyo aliongeza kuwa msimu wake wa kwanza kucheza ligi ya Tanzania akitaja ni miongoni mwa ligi ngumu ambayo inaweza kumwongezea uzoefu mchezaji.

“Tulicheza dhidi ya Simba na Yanga ni timu nzuri na tulipokutana nao ilikuwa mechi yenye ushindani sana ni mara yangu ya kwanza kukutana nao na nimejifunza vitu vingi binafsi kwa sababu ni kipa ninahitaji kuwa makini langoni,” amesema Chelsea na kuongeza;

“Mechi hizo zimenishtua natakiwa kupambana kuhakikisha kila mechi ninapata nafasi ya kucheza basi tusiruhusu mabao kwa sababu WPL ni ligi ngumu sana.”

Kwenye mechi sita alizocheza Chelsea ameruhusu mabao 10 Tausi ikiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi na pointi mbili.

Chelsea ni golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Cameroon U-20, na pia ni sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa.