KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema sababu kubwa ya timu hiyo kutofanya vizuri mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake ni kukosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao.
Ceasiaa ipo mkiani mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi mbili pekee baada ya kucheza mechi nane hali ambayo imewalazimu benchi la ufundi kufanya tathmini ya kina ili kujiokoa kwenye msimamo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chobanka amesema dirisha dogo la usajili wanafanya marekebisho na wako kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji mmoja kutoka Uganda anayeamini ataongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
“Tatizo letu kubwa ni upande wa mbele mabeki wanajitahidi kufanya kazi yao, lakini tunapofika eneo la kufunga, bado tunapata changamoto kubwa, kuna mchezaji wa Uganda ambaye tuko naye kwenye mazungumzo ya mwisho, tukikamilisha usajili wake na kama akizoea mazingira mapema atatusaidia sana,” amesema Chobanka.
Kocha huyo pia alibainisha timu hiyo ina matumaini makubwa iwapo taratibu za vibali kwa wachezaji wawili kutoka Kenya zitakamilika mapema.
“Endapo viongozi wetu watakamilisha taratibu za vibali vya Anitha Adongo na Cherono ni wachezaji wazuri wenye uzoefu, wanaweza kutupa nguvu kubwa hasa kwenye ushindani wa ligi.”
Chobanka alisisitiza Ligi Kuu ya Wanawake imekuwa na ushindani mkubwa msimu huu na kila msimu unakuja na sapraizi zake, lakini bado wana nafasi ya kupambana na kusogea juu ya msimamo iwapo wataweka mikakati sahihi.
“Ligi bado mbichi, ushindani ni mkubwa lakini bado tuna mechi nyingi mbele yetu, kama tutarekebisha mapungufu
na kuweka mipango vizuri, tuna uwezo wa kuwa katika nafasi nzuri.”