Nashon: AFCON imeniongezea kitu | Mwanaspoti

KIUNGO mkabaji wa Pamba Jiji, Kelvin Nashon amesema mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2025 yaliyomalizika jana huko Morocco, yamemwongezea uzoefu na kujiamini, jambo ambalo litamsaidia katika Ligi Kuu Bara.

Nashon alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michuano hiyo Morocco na kuishia hatua ya 16 bora (mtoano) ambayo waliondolewa na wenyeji Morocco kwa kufungwa bao 1-0.

Kiungo huyo anayecheza Pamba Jiji kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, hakucheza mechi yoyote kati ya mechi nne ambazo Taifa Stars ilicheza amejiunga na kambi ya timu yake kwa ajili ya maandalizi ya ngwe ya Ligi Kuu Bara

Akizungumza baada ya kuungana na wenzake kambini jijini Mwanza, Nashon amesema uzoefu alipokutana nao akiwa na Serengeti Boys mwaka 2017 kule Gabon ni tofauti na sasa, kwani kipindi kile alikuwa anajitafuta lakini sasa amekutana na nyota wenye majina na uzoefu mkubwa ndani na nje ya Afrika.

“Wakati huu nimeenda kama mchezaji senior (mzoefu) nimekutana na wachezaji wakubwa wanaocheza klabu kubwa   duniani, unaona wanavyocheza unakutana nao unaona mtindo wao wa maisha, inakusaidia kuamini kumbe inawezekana tu hata sisi tukipambana ikawa,” amesema Nashon.

NASHO 01


Amesema licha ya kutopata nafasi ya kucheza katika michuano, lakini naamini amejifunza kitu na kupata uzoefu utakaomsaidia wakati mwingine atakapohitajika kwenye timu ya taifa.

“Kujiamini kwangu kumeongezeka bila kujali kama sikupata namba kwa sababu ya muda na mechi chache. Kilichotokea kimenijenga kwani tulitengeneza umoja, malengo na kiu ya kufanya vizuri na kufika mbali, pia nilijifunza kwa wachezaji waliokuwa walicheza nafasi yangu,” amesema Nashon na kuongeza;

“Watanzania au wana Pamba wategemee kuniona wa tofauti kwani madini nimeyapata, kama nimeweza kwenda kucheza mashindano makubwa kama yale katika ligi sidhani kama nitashindwa, kwani nimeongeza ari kubwa ya kujiamini ya kuikabili timu na mchezaji yeyote bila hofu, hivyo tutegemee nitacheza kwa confidence (kujiamini) kubwa sana.”

Akizungumzia ukarimu alioonyeshwa na wenzake kwa kukaribishwa mazoezini, Nashon aliwashukuru Pamba Jiji, huku akiamini upendo huo ni deni kwake ambalo anapaswa kulilipa kwa kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake msimu huu.

NASHO 02


“Ni kitu ambacho sikutarajia yaani kwa upendo huu naweza nikasema Pamba wanazidi kuniongezea mzigo mkubwa sana, wananiongezea deni kubwa kwamba kuna timu unaweza ukawa   unacheza lakini kuna familia, sasa hii imekuwa ni zaidi ya timu hii ni familia,” amesema Nashon.

Pamba Jiji ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ikiwa pointi 16 kama ilizonazo Yanga licha ya kutofautiana mabao ya kufungwa na kufungwa nyuma ya JKT Tanzania yenye pointi 17.