Asilimia 74 hawajaripoti kidato cha kwanza Mara

Musoma. Asilimia 26.43 ya wanafunzi wote wa kidato cha kwanza waliotarajiwa kuripoti kwa ajili ya kuanza masomo ya elimu ya sekondari kwa kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za umma mkoani Mara, ndio wamekwisha ripoti shuleni hadi sasa.

Pia asilimia 85.07 ya wanafunzi waliotarajiwa kuanza darasa la kwanza katika shule za msingi za umma mkoani Mara ndio wamekwisha ripoti, huku kwa upande wa darasa la awali asilimia 67.34 ndio wamekwishaanza masomo.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mara, Dk Elpidius Baganda amelimbia Mwananchi leo Jumapili Januari 18,2026 kuwa takwimu hizo za wanafunzi walioripoti shuleni ni za hadi Ijumaa Januari 16,2026.

Amesema kwa mujibu wa takwimu mkoa huo unatarajiwa kupokea wanafunzi 41,516 kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka huu katika shule za sekondari za umma lakini hadi sasa walioripoti ni wanafunzi 10,973 pekee.

Amesema kwa darasa la kwanza mkoa ulikuwa na maoteo ya kuandikisha wanafunzi 102,269 na   hadi sasa jumla ya wanafunzi 60,579 ndio walioanza masomo.

Kwa upande wa darasa la awali, Dk Baganda amesema mkoa huo ulikuwa na maoteo ya kuandikisha wanafunzi 85,475 ambapo hadi sasa waliopo shuleni ni wanafunzi 57,556.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza wanafunzi wote wa madarasa hayo kuripoti shuleni ifikapo kesho Jumatatu Januari 19, 2026.

Akiwa wilayani Rorya , Mtambi amesema baada ya Januari 19,2026 msako mkali utaanza ukihusisha nyumba kwa nyumba na kuwakamata wazazi ambao wameshindwa kuwapeleka watoto wao shule.

Amesema Serikali mkoani humo tayari imetoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote kuwapokea wanafunzi wote katika hali yoyote ile hata kama hawana mahitaji muhimu kama vile sare za shule.

Amesema wakati wazazi wakikamilisha mahitaji hayo ya shule wanafunzi hawapaswi kuzuiliwa kuendelea na masomo, huku akisema kuwa kwa wale wa kidato cha kwanza wanaruhusiwa kwenda shuleni hata wakiwa wamevaa sare zao za shule ya msingi.

Amesema msako wa kuwatafuta wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni utaongozwa na diwani na mwenyekiti wa serikali wa eneo husika sambamba na watendaji wa Serikali waliopo katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine amemuagiza msimamizi wa mradi wa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (Veta) wilayani Rorya kuhakikisha   unakamilika ndani ya mwezi huu ili kuruhusu wanafunzi kuanza masomo chuoni hapo ifikapo Februari .

Kanali Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kutokuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ulioanza   mwaka 2023 kwa gharama ya zaidi ya Sh1.4 bilioni.

“Mwaka huu mkoa wetu umefanya vibaya kwenye mtihani wa darasa la saba, hii ina maana wapo watoto ambao wamemaliza darasa la saba lakini hawataenda sekondari sasa mnataka   waende wapi kama sio kwenye vyuo vya ufundi kama hivi ili wapate ujuzi, nataka hiki chuo kianze kuchukua wanafunzi Februari mwaka huu,” amesema

Akitoa taarifa ya mradi huo, Ofisa Mthibiti Ubora wa Elimu Wilaya ya Rorya, Masanja Mashimba amesema hadi sasa umefika asilimia 57 za utekelezaji wake .

Amesema zipo changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji na umeme wa uhakika.

Kuhusu changamoto hizo Mtambi,  amewaagiza Meneja wa Tanesco (Shirika la Umeme) pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) mkoani humo kupeleka huduma hizo katika eneo hilo ndani ya wiki moja.

Wakizungumza kuhusu kasi ndogo ya wanafunzi kuripoti shuleni baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara wamesema zipo sababu mbalimbali ikiwepo uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

“Unajua wapo baadhi ya wazazi wanawatumia watoto wao kama kitega uchumi, yaani akimaliza tu darasa la saba anatafutiwa kibarua kwa lengo la familia kujipatia kipato kwa hiyo mzazi anaona ule ujira wa mtoto ni wa maana sana kwenye familia kuliko elimu, ” amesema Robert Mujungu.

Mujungu amesema watoto hao wanatumiwa na wazazi katika kufanya biashara ndogondogo ama wengine kutafutiwa kazi za ndani hasa wale wanaotoka vijijini ambao wengi wao hupelekwa mijini.

Annamaria Mseti amesema uwepo wa shughuli za uchimbaji madini na uvuvi ndani ya mkoa huo pia ni sababu ya kuwepo kwa idadi ndogo ya wanafunzi shuleni, kwani wapo baadhi yao ambao wanakwenda katika maeneo hayo kwaajili ya kutafuta ajira za muda ili kujipatia kipato.

“Lakini pia kuna wazazi wameamua kuwapeleka watoto wao shule binafsi,hili nalo lina mchango katika hili la wanafunzi wachache kuripoti kidato cha kwanza,” amesema Benjamin Wegesa

Amina Mohamed ameomba hatua kali zichukuliwe kwa wazazi ambao wanakuwa kikwazo kwa watoto wao kupata elimu kwa maelezo kuwa hivi sasa hakuna sababu ya mtoto kushindwa kusoma, kwani Serikali inabeba gharama kubwa kwabajili ya elimu ya watoto.