Simba imeendelea kukutana na matokeo mabaya kwenye michezo ya Ligi Kuu msimu huu baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwenye ligi kwa timu hiyo baada ya kupita zaidi ya mwezi mmoja na ulifanyika kwenye Uwanja wa Meja Isamhuyo Mbweni jijini Dar es Salaam, sehemu ambayo timu hiyo ya Msimbazi inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.
Kabla ya mchezo huu, Simba ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam kwenye mchezo mwingine wa ligi, hali ambayo kwa sasa inawaweka kwenye wakati mgumu kuwania ubingwa msimu huu.
Simba ambaye ilicheza chini ya kocha mpya Steven Barker, ilikuwa ya kwanza kujipatia kwenye mchezo huo katika dakika ya 19 ya mchezo, baada ya Elli Mpanzu kufunga kwa shuti kali ndani na eneo la hatari baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Shomary Kapombe.
Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo ambapo ilifanikiwa kujipatia bao la kusawazisha katika dakika ya 61 kupitia kwa Fredrick Magata aliyefunga kwa shuti ambalo lilimshinda kipa wa Simba Hussein Abel, ambaye amedaka kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye ligi msimu huu.
“Kiwango hiki siyo sahihi kwa timu kubwa kama Simba, tunatakiwa lazima kubadilika haraka sana, tunakwenda kwenye mazoezi kuhakikisha hali hii inabadilika haraka,” alisema kocha wa Simba Barker.
Kwa upande wa kocha wa Mtibwa Yusuf Chippo alisema timu yake imecheza vizuri kwenye mchezo huu.
Matokeo haya yanaifanya Simba kuwa na pointi 13, katika nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya kucheza michezo sita.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar yenyewe imesogea hadi nafasi ya nane ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza michezo tisa.