Dodoma. Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umeme (ETDCO) imesaini mikataba ya kutekeleza miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ya kusambaza umeme katika vitongoji 620 vya mikoa ya Katavi na Ruvuma, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 95.2.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Jumapili, Januari 18, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesisitiza umuhimu wa uadilifu na usimamizi thabiti ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Ndejembi amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa REA, Mhandisi Hassan Said amewataka makandarasi kuzingatia ubora wa kazi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwapatia Watanzania huduma ya umeme ya uhakika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja ameishukuru Wizara ya Nishati pamoja na REA kwa imani waliyoipa kampuni hiyo, huku akieleza kuwa ETDCO imejipanga kutekeleza miradi kwa wakati na kuzingatia masharti ya mikataba.
Amesema miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu na itanufaisha wananchi wa awali takribani 19,950 katika mikoa ya Katavi na Ruvuma.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 500 ikiwemo za moja kwa moja, huku wananchi wa maeneo husika wakihimizwa kuchangamkia fursa hizo.
Kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa za kijamii na kiuchumi, kuimarisha shughuli za maendeleo, na kuchangia ustawi endelevu wa Taifa.