Dira 2050 kuwakutanisha wadau wa Tehama, mambo matano kujadiliwa

Dar es Salaam. Wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wanatarajia kukutana kesho Januari 19, 2026 jijini Dar es Salaam ambapo watajadili mambo matano muhimu ikiwa ni hatua za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo (Dira 2050).

Kongamano hilo la tisa la mwaka (TAIC-2026) lililoandaliwa na Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuelekeza namna uchumi wa kidijitali utakavyokuwa injini kuu ya utekelezaji wa dira hiyo.

Akizungumzia mkutano huo leo Januari 18, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dk Nkunde Mwasaga amesema mapinduzi ya kidijitali yana nguzo tano ambazo ni ujuzi wa kidijitali unaohusisha matumizi ya mifumo na vitu vyote vinavyohusiana na masuala ya kidijitali.

“Elimu ya msingi ya kidijitali kwa wananchi wote ambapo kila Mtanzania anapaswa kuwa na uwezo wa kutumia mifumo na zana za kidijitali. Pili, ni wataalamu wa kati ambao watasaidia watu kutatua changamoto zitakazojitokeza kwenye mifumo mbalimbali.

Amesema ujuzi wa kati na wa juu wa kidijitali, ikiwemo mafundi na wataalamu wa ngazi ya juu wanaoweza kubuni na kuendesha mifumo ya kisasa, hususan inayotumia akili unde (AI).

Maeneo mengine muhimu yatakayojadiliwa ni usalama wa mtandao na faragha ya taarifa, upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma, pamoja na mchango wa tafiti, ufadhili na mifumo ya biashara katika kuendeleza uchumi wa kidijitali.

Hayo yanajiri wakati Tanzania ikijiandaa kuanza rasmi safari ya miaka 25 ya maendeleo chini ya Dira ya Taifa ifikapo Julai Mosi, 2026.

Hata hivyo, kongamano hilo la siku tano kuanzia kesho Jumatatu Januari 19 hadi Ijumaa Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam, linafanyika katika kipindi ambacho Taifa limeweka wazi mageuzi ya kidijitali ni mhimili mkuu wa ukuaji wa uchumi, ujumuishi wa kijamii na ushindani wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Dk Mwasaga, mageuzi ya kidijitali yametambuliwa wazi katika dira hiyo kama kichocheo kikuu cha kuharakisha ukuaji wa uchumi kuelekea azma ya muda mrefu ya uchumi wa dola trilioni moja.

Kwa upande wa sekta binafsi, Joseph Muhavile, mjasiriamali wa teknolojia, amesema fursa ya kukutana na wataalamu wa kimataifa ni moja ya nguvu kubwa ya mkutano huo.

“Kuwa na wataalamu kutoka nje kunatupa nafasi ya kujifunza kutoka kwa mataifa yaliyofanikiwa kutumia teknolojia kukuza uchumi wao. Pia, inatuma ujumbe kuwa Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji wa kidijitali na ushirikiano,” amesema.