Depu, Okello kuanza kujibu maswali magumu Yanga

LAURINDO Dilson Maria Aurélio maarufu kwa jina la Depu sambamba na Allan Okello, wameyaanza maisha yao mapya ndani ya Yanga sambamba na nyota wengine waliosajiliwa dirisha dogo la usajili msimu huu.

Nyota wengine ni Emmanuel Mwanengo na Mohamed Damaro ambao wametambulishwa na kukiwasha kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 wakibeba taji hilo ikiifunga Azam kwa penalti 5-4.

Wakati Mwanengo na Damaro wakikichafua, Okello na Depu bado huku wakionekana mazoezini wakijifua na wenzao na huenda leo Jumatatu ikawa shoo yao ya kwanza katika Ligi Kuu Bara kama mambo yatakwenda vizuri.

Yanga inayofundishwa na Pedro Goncalves, leo Jumatatu itakuwa mwenyeji wa Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Ni mechi ambayo Yanga inahitaji zaidi ushindi ili kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 19, na kuishusha JKT Tanzania yenye 17 baada ya kucheza mechi 10. Yanga itakuwa ni mechi yake ya saba.

Kwa upande wa Mashujaa, nayo inasaka ushindi ili kufikisha pointi 16 ilizonazo Yanga hivi sasa, lakini rekodi zinainyima timu hiyo kufurukuta.

Huu ukiwa ni msimu wa tatu Mashujaa inashiriki Ligi Kuu Bara, haijawahi kupata hata sare mbele ya Yanga, imepoteza zote iwe nyumbani au ugenini.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa KMC, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2, ilikuwa Desemba 19, 2024. Baada ya hapo, Yanga ikashinda 5-0 nyumbani kwa Mashujaa, Fberuari 23, 2025.

Mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo Februari 8, 2024, Yanga ilishinda 2-1 nyumbani, kisha ikaenda kushinda 1-0 ugenini, Mei 5, 2024.

Hii itakuwa mechi ya kumi kwa Pedro katika mashindano tofauti tangu atue Yanga Novemba 5, 2025 ikishuhudiwa ushindi mara nane na sare moja. Hajapoteza.

Katika mechi tisa alizoongoza Yanga, timu hiyo imeshinda zote tatu za Ligi Kuu Bara, nne za Kombe la Mapinduzi, moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na sare ni michuano hiyo pia.

Licha ya Mashujaa rekodi kuwakataa, lakini lolote linaweza kutokea katika dakika tisini za mechi hiyo ambayo Yanga itaicheza huku ikiiwaza Al Ahly itakayokutana nayo Ijumaa katika mechi ya kundi B kunako Ligi ya Mabingwa Afrika ikicheza Misri.