Kiongozi Mkuu wa Iran Amshutumu Trump kwa Vifo vya Waandamanaji – Video


Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, siku ya Jumamosi amemlaumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa wiki kadhaa za maandamano nchini Iran ambayo, kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadamu, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.

Akizungumza kupitia vyombo vya habari vya serikali ya Iran, Khamenei alisema kuwa Iran inamchukulia Rais wa Marekani kama mhalifu kwa kile alichokitaja kuwa vifo, uharibifu na kashfa zilizosababishwa kwa taifa la Iran.

“Tunamchukulia rais wa Marekani kuwa mhalifu kwa vifo, uharibifu na fedheha alizolisababishia taifa la Iran,” alisema Khamenei.

Kauli hiyo inakuja huku Trump akiendelea kutoa vitisho vya kuingilia kati hali ya kisiasa ya Iran, ikiwa ni pamoja na kauli za kutishia kuchukua “hatua kali sana” endapo serikali ya Iran ingewanyonga waandamanaji.

Hata hivyo, siku ya Ijumaa, Trump aliandika ujumbe katika mitandao ya kijamii akiwashukuru viongozi wa Tehran kwa kile alichodai kuwa kufutwa kwa mpango wa kunyonga waandamanaji. Serikali ya Iran ilikanusha vikali madai hayo, ikisisitiza kuwa hakukuwa na mpango wa kuwanyonga watu.

Katika kile kilichotafsiriwa kama jibu la moja kwa moja kwa Trump, Khamenei alisema Iran haitaki kuingia vitani, lakini haitowaacha wale aliowataja kuwa wahalifu wa ndani au wa kimataifa bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hatutaivuta nchi kwenye vita, lakini hatutawaacha wahalifu wa ndani au wa kimataifa waende bila kuadhibiwa,” alinukuliwa Khamenei.