Fei Toto amebakiza mawili tu Bara

BAO la pili lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika dakika ya 35 wakati timu hiyo ikiizamisha Coastal Union kwa mabao 3-0 juzi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam limezidi kumpaisha nyota huyo katika Ligi Kuu Bara.

Azam ilipata ushindi huo uliokuwa ni wa tatu kwa timu hiyo msimu huu na kuifanya ifikishe pointi 12 na kuchupa kutoka nafasi ya tisa hadi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo, huku Fei Toto akifikisha bao la tatu msimu huu, mbali na asisti mmoja aliyonayo hadi sasa.

Mabao mengine katika mchezo huo ulioifanya Azam kuendeleza kubabe mbele ya Wagosi wa Kaya yaliwekwa kimiani na Yahya Zayd aliyefunga kwa penalti dakika ya 24 na Japhte Kitambala aliyekwamisha sekunde chache kabla ya mapumziko na kumfanya afikishe bao la pili la Ligi Kuu.

Hata hivyo, kama hujui ni bao alililofunga Fei Toto, limemfanya afikishe jumla ya mabao 48 katika Ligi Kuu tangu aanze kucheza mwaka 2018 alipojiunga na Yanga kutokea JKU ya Zanzibar na kuitumikia kwa misimu mitano kabla ya kujiunga na Azam misimu mitatu iliyopita.

FEI 01


Hii ina maana nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania aliyewaka katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizomalizika jana akiwa na Taifa Stars na aliyechaguliwa kuwa nyota wa mechi ya juzi, sasa amebakiza mabao mawili tu kufikisha mabao 50, huku akiwa amefunga katika misimu nane mfululizo.

Akiwa na Yanga aliyoitumikia kwa misimu mitano kabla ya kulazimisha kuhama kujiunga na Azam FC aliifungia jumla ya mabao 22, huku misimu mitatu akiwa na Azam amefunga mabao 26 katika mechi zaidi ya 100, zikiwamo 55 akiwa na timu ya sasa iliyomwogezea mkataba hadi 2027.

Fei Toto ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao kama atafunga katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate kabla ya timu kusafiri kwenda Nairobi kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao, Nairobi United.

Azam inashiriki hatua ya makundi kwa mara ya kwanza na ilianza vibaya kwa kupoteza mechi mbili za awali za Kundi B dhidi ya AS Maniema ya DR Congo na Wydad Casablanca ya Morocco na itacheza na Nairobi United inayoburuta mkia wa kundi hilo Januari 25 kisha kurudiana nao Februari Mosi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar inayoutumia kama nyumbani.

Rekodi zinaonyesha msimu wa kwanza akiwa na Yanga, Fei Toto alifunga mabao manne tu, kisha msimu wa 2019-2020 alifunga bao moja na msimu uliofuata alifunga mabao matano na misimu miwili ya mwisho alifunga mabao sita kila mmoja na katikati ya msimu alianzisha mgomo kushinikiza kuhamia Azam FC kabla ya Rais Samia Suluhu kuingilia kati Yanga ikiwa Ikulu.

FEI 02


Rais Samia aliyekuwa akiipongeza Yanga kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 2-2 na USM Alger ya Algeria, aliutaka uongozi wa klabu hiyo kumruhusu aende atakapo na siku moja baadae ilitangazwa biashara ya Yanga kumalizana na Azam anayoichezea hadi sasa.

Akiwa na Azam, msimu wa kwanza alifunga mabao 19 akishika nafasi ya pili ya Wafungaji Bora nyuma ya kinara, Stephane Aziz Ki aliyekuwa Yanga enzi hizo na msimu uliopita alifunga manne na kwa msimu huu amefunga matatu na kumfanya afikishe mabao 26 hadi sasa katika misimu mitatu akiwa Azam, manne zaidi na yale aliifungia Yanga kupitia misimu mitano aliyoitumikia.

Mbali na mabao 48 katika Ligi Kuu, pia Fei Toto amehusika na mabao mengine zaidi ya 50 kutokana na asisti alizotoa kwa wenzake kwa timu hizo mbili, zikiwamo 13 za msimu uliopita akiwa ndiye kinara katika ligi hiyo, japo msimu huu ameasisti mara moja kupitia mechi sita.