KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Zuwena Aziz ‘Zizou’, anayekipiga katika timu ya Mogbwemo Queens ya Sierra Leone ametaja utofauti wa ligi ya nchi hiyo na Tanzania.
Zizou ambaye alijiunga na Mogbwemo Queens akitokea Tausi (zamani ikiitwa Ukerewe Queens), aliitumikia kwa msimu mmoja na kuipandisha Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zizou amesema jambo la kwanza ni namna mashabiki wanavyosapoti timu na kujaa uwanjani, tofauti na Tanzania ambako bado hakuna mwamko mkubwa wa mashabiki.
“Hapa mashabiki wanajaa uwanjani kama vile ni mechi za wanaume. Wana ushabiki mkubwa na wanajua kuhamasisha timu zao. Ni tofauti na Tanzania, viwanja vya soka bado vinahitaji kuboreshwa kwa ajili ya kuzingatia kiwango cha kisasa,” amesema Zizou na kuongeza;
“Wachezaji wa kike wanapewa kipaumbele hapa Sierra Leone, wanathaminiwa na wanapata fursa nzuri jambo linalowafanya waendelee kujituma na kuonyesha vipaji vyao, kwetu kidogo changamoto.”
Nyota huyo wa zamani wa Thika Queens ya Kenya aliongeza hadi sasa changamoto kwake ni lugha kwani asilimia kubwa ya wachezaji wanazungumza Krio (lugha ya taifa lao).
“Hapa wanazungumza Krio na Kiingereza kidogo, lakini kwa upande wangu naelewa kwa vitendo zaidi. Ingawa lugha inaweza kuwa changamoto kidogo, lakini najitahidi kuelewa hasa zile lugha za mpira.”