Ajali treni ya mwendokasi yaua 21 Hispania

Hispania. Watu 21 wamepoteza maisha na wengine 30 wakijeruhiwa baada ya treni mbili za mwendokasi kugongana nchini Hispania, mamlaka za nchi hiyo zimethibitisha.

Kwa mujibu wa DW na Al Jazeera, ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Januari 19, 2026, karibu na mji wa Adamuz mkoani Andalusia ambapo mkia wa treni iliyokuwa ikitoka Malaga kuelekea Madrid, ikiwa na takribani abiria 300, ulitoka kwenye reli saa 1:45 usiku na kugonga treni nyingine iliyokuwa ikitoka Madrid kwenda Huelva ikiwa na abiria 200.

Waziri wa Uchukuzi wa Hispania, Oscar Puente amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika, akieleza kuwa ni jambo la kushangaza kwa treni kutoka kwenye reli katika eneo la reli lililo nyoofu. Ameongeza kuwa reli hiyo ilifanyiwa ukarabati Mei 2025.

Kwa mujibu wa Shirika la Reli la Hispania (ADIF), ajali hiyo ilisababisha majeruhi wengi huku kituo cha televisheni ya umma nchini humo cha Television Espanola, kikiripoti dereva wa treni iliyokuwa ikitoka Madrid kwenda Huelva ni miongoni mwa waliofariki.

Ripoti zinaeleza kuwa jumla ya watu 100 walijeruhiwa ambapo 30 kati yao wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya. Juhudi zilielekezwa kuwahudumia na kuwatuliza majeruhi kabla ya kuwapeleka hospitalini.

Rais wa serikali ya Mkoa wa Andalusia, Juanma Moreno amesema katika mitandao ya kijamii kuwa huduma katika eneo la tukio zilikuwa zikishirikiana kwa karibu na vyombo vya msaada wa dharura, akitoa pole kwa waathirika wote wa ajali hiyo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez amesema taifa hilo limeingia katika usiku wa maumivu makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya ya treni.

Kupitia mtandao wa X, Sanchez ametuma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu wa marehemu, akisisitiza kuwa nchi nzima iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

Kutokana na ajali hiyo, safari za treni kutoka Andalusia kwenda Madrid zimesitishwa. Shirika la reli limesema huduma kutoka Cordoba, Sevilla, Malaga na Huelva hazitapatikana hadi Jumatatu ijayo.

Mmoja wa manusura wa ajali hiyo, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha RTVE, Salvador Jimenez, aliyekuwa ndani ya treni ya Malaga, amesema behewa mbili za mwisho zilitoka kwenye reli huku behewa la mwisho likianguka ubavuni kabisa.

Amesema kabla ya ajali, treni ilikuwa kama inapitiwa na tetemeko la ardhi. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo iliyotikisa Hispania na kuacha taifa likiwa katika majonzi.