Itigi. Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ameagiza hatua kali zichukuliwe kwa Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Itigi kutokana na tuhuma za rushwa.
Kihongosi alitoa agizo hilo jana jioni Jumapili Januari 18,2026 alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya stendi ya zamani.
Mganga huyo alilalamikiwa na watu zaidi ya watatu kila mmoja akieleza namna wanavyotozwa fedha kwa huduma ambazo hazistahili kutozwa lakini hawapewi risiti.
Hata hivyo, jana Kihongosi alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk James Bwire kuwalipa watu wawili ambao walithibitisha kudaiwa Sh28,000 jambo lililotekelezwa papo hapo.
“DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) nataka ulipe fedha za hawa watu ili ikuume zaidi na uanze kuchukua hatua kwa mtu wako ambaye hakuja kwenye mkutano na nitapokea utekelezaji wake kabla sijamaliza ziara yangu mkoani Singida,” alisema Kihongosi na kushangiliwa kwa nguvu.
Kiongozi huyo aliwataka watumishi wanaopewa dhamana ya kusimamia maeneo wafanye kazi kwa weledi huku wakitambua kuwa waajiri wao ni wananchi.
“Kuna watu wanapewa dhamana ya kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi lakini wanajigeuza kuwa miungu watu, wanaomba rushwa, wanatoa lugha chafu kwa wanaowahudumia lakini uwajibikaji wao ni matatizo, wanagombanisha Serikali na wananchi, hawa wasivumiliwe,” aliagiza.
Katika hatua nyingine Kihongosi amekutana na malalamiko ya wananchi wa Kitongoji cha Majengo katika Wilaya ya Manyoni wakidai kuchukuliwa ardhi yao na Serikali ambayo imejenga chuo lakini hawajalipwa fidia ya namna yoyote.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dengedo alikiri kuwepo kwa jambo hilo lakini akasema wanalifanyia kazi ambapo aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati jambo lao linashughulikiwa.
“Mheshimiwa Mwenezi, ni kweli ardhi ya wananchi hawa imechukuliwa kwa ajili ya kujenga Chuo cha Veta, nilishawaambia wananchi hakuna atakayepoteza haki yake, nakuja hapa Januari 24,2026 ili kuzungumza nao na tutayamaliza,” alisema Dendego.
Mbunge wa Itigi, Yohana Msita alimwambia Katibu wa huyo kwamba wananchi wa maeneo hayo wanadai fidia ya upishaji wa ujenzi wa reli ya mwendo kasi (SGR) kwa muda mrefu, lakini hawajalipwa na hawajui hatima yao zaidi ya kusimamishwa wasifanye maendelezo hata majengo yaliyoharibika.