40 wajitokeza kuwekeza sekta ya bidhaa za afya Tanzania

Dar es Salaam. Wawekezaji 40 wamejitokeza kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za afya nchini Tanzania, huku 25 kati yao wakihudhuria mkutano maalumu uliowakutanisha wadau wa Serikali na sekta binafsi, wakitoka katika mataifa mbalimbali.

Baadhi ya wawekezaji hao wanaotarajia kuanzisha viwanda vya bidhaa za afya nchini wametoka katika nchi za  Dubai, Misri, Ujerumani, Somalia, Sudan Kusini, Kenya, China, Rwanda, Ethiopia na India.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 19, 2025 wakati wa Jukwaa la Uwekezaji wa Bidhaa za Afya Tanzania, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amezitaja nchi hizo akisema Tanzania inaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta ya afya, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora za afya na kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa hizo ndani na nje ya mipaka yake.

“Leo tumefanikiwa kuwa na wawekezaji 40 na katika mkutano huu wamehudhuria 25, kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Dk Magembe na kuyataja mataifa hayo.

Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa akisalimiana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe wakati akiwasili kwenye Jukwaa la Uwekezaji wa Bidhaa za Afya Tanzania, linalofanyika jijini Dar es Salaam.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Viwanda vya Dawa Tanzania (TPMA), Bashiru Haruna, amesema kuundwa kwa kikosi kazi cha kushughulikia masuala ya uwekezaji kumechangia kuweka mwelekeo sahihi na kujenga mazingira mazuri ya kukuza viwanda vya bidhaa za afya.

Amebainisha kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii wa tiba.

“Tunawakaribisha wawekezaji wa nje kuungana nasi. Sisi wawekezaji wa ndani tunatarajia kuunganisha nguvu ili tukue pamoja na kufikia malengo ya pamoja. Tupo hapa kuhakikisha Tanzania inafanikisha malengo yake, karibu katika soko hili kubwa tufanye kazi kwa karibu na Serikali yetu,” amesema Haruna.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dk Emmanuel Nuwasi, amesema Bunge litaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha Tanzania inakuwa mzalishaji na msambazaji wa bidhaa za afya kwa soko la ndani na la kimataifa.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zitalenga kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za kutosha, sambamba na kusimamia ipasavyo masuala ya kisheria ili kulinda uwekezaji.

Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, amesema changamoto zilizojitokeza wakati wa janga la UVIKO-19 zilidhihirisha umuhimu wa Tanzania kuzalisha bidhaa zake za afya badala ya kutegemea uagizaji kutoka nje.

Amesema kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP), Serikali imeandaa mfumo wa kisheria wa PPP Act ya mwaka 2023 ili kuwezesha na kulinda fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tanzania ina dhamira ya kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa bidhaa bora za afya. Tuko wazi kwa ushirikiano na tayari kufanya kazi nanyi katika utekelezaji, ili kuzalisha ajira, kuhamisha teknolojia kwa Watanzania na kuchangia maendeleo ya Bara la Afrika,” amesema Munde.

Hatua hiyo inaonesha mwelekeo mpya wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya afya kama nguzo ya maendeleo ya viwanda na uchumi kwa ujumla.

Jukwaa hilo la uwekezaji linaloendelea kufanyika jijini Dar es Salaam, litajumuisha majadiliano mbalimbali miongoni mwa wataalamu wa bidhaa za afya ndani na nje ya nchi.