LHRC yafungua kesi kupinga adhabu ya viboko shuleni

Arusha. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Kuu -Dodoma, kupinga uhalali wa matumizi ya adhabu ya viboko shuleni, Tanzania Bara.

Kesi hiyo imewasilishwa kwa niaba ya Samwel Maduhu, ambaye ni mlezi aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasamba mkoani Simiyu, Mhoja Maduhu (marehemu kwa sasa).

Mhoja alidaiwa kufariki akidaiwa kupigwa na mwalimu wake kwa fimbo, ikiwemo kichwani alipokuwa akijaribu kujikinga.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na LHRC mwishoni mwa wiki, imeeleza kuwa Kituo hicho kinamwakilisha mlalamikaji kama sehemu ya jitihada zake endelevu za kulinda haki za watoto na kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa salama na yenye heshima.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kesi hiyo inapinga Kanuni ya 2, 3 na 6 za Kanuni za Elimu (Adhabu ya Viboko), GN. Na. 294 ya 2002, kwa hoja kwamba zinakiuka Katiba hususan haki ya heshima na utu, haki ya kusikilizwa, na haki ya kuwa huru dhidi ya mateso au adhabu au matendo ya kikatili au ya kudhalilisha.

Kwa mujibu wa taarifa kesi hiyo imepewa namba 32373/2025 na imepangiwa kusikilizwa mbele ya majaji watatu ambao ni Amir Mruma, Hassan na Irene Musokwa.

Imefafanua kuwa kesi hiyo imepangwa kutajwa Machi 16,2026 saa tatu asubuhi, ambapo Kituo hicho kimeeleza kuwa kitaendelea kufuatilia shauri hilo kwa karibu, kuhakikisha haki inapatikana kwa Mhoja na kuendeleza msukumo wa mageuzi ya kisheria yanayolinda watoto dhidi ya adhabu za kikatili na za kudhalilisha shuleni.

Imeeleza kuwa shauri hili linatokana na tukio hilo la kusikitisha ambapo Mhoja na wenzake waliadhibiwa kwa kutokamilisha kazi ya somo la Jiografia kinyume na maelekezo ya walimu.

Mhoja alipigwa mara kadhaa kwa fimbo, zikiwemo viboko viwili kichwani alipokuwa akijaribu kujikinga, ambapo alidaiwa kuanguka chini  hali yake ikazidi kuwa mbaya, na licha ya kulia kwa maumivu, mwalimu aliendelea kumsukuma kichwani ili amnyamazishe.

Ilidaiwa kuwa alikimbizwa hospitalini lakini alifariki dunia ambapo ripoti ya uchunguzi wa mwili ilionyesha kuwa alikufa kutokana na kutokwa na damu ndani ya fuvu la kichwa baada ya kupigwa na kitu butu.

Taarifa hiyo imesema kuwa mwalimu aliyempiga mwanafunzi huyo alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuua bila kukusudia katika shauri la jinai namba 16680/2025,Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Shinyanga ambapo alikiri kosa hilo na  kuhukumiwa adhabu ya kutotenda kosa lolote ndani ya kipindi cha miezi 12.

Mwanafunzi huyo wa kike, kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake, tukio lililotokea Februari 26,2025 baada ya mwalimu huyo kutoa kazi ya vikundi kwa wanafunzi wa darasa hilo, ambapo baadhi yao hawakuifanya akiwemo marehemu.

Mmoja wa wanafunzi alidai ambao hawakufanya kazi hiyo walitolewa nje ya darasa na kupewa adhabu ya kupiga magoti kabla ya kuanza kuchapwa viboko 10 kila mmoja na kuwa Maduhu alipigwa fimbo za kichwani na mgongoni kisha kukanyagwa.