Tanga. Wizara ya Fedha imesema inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanakuwa wamepata elimu ya fedha, ikilinganishwa na asilimia 53.5 ya sasa kwa mujibu wa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dionisia Mjema, wakati wa kikao na waandishi wa habari jijini Tanga kuelekea ufunguzi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa itakayofanyika kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026.
Mjema amesema utafiti wa upatikanaji wa huduma za fedha umefanyika kwa awamu mbalimbali kuanzia mwaka 2006, 2009, 2013, 2017 hadi 2023, na kubaini kuwa ni asilimia 53.5 tu ya wananchi wanaotumia huduma rasmi za fedha ikiwemo benki za biashara, bima na huduma za fedha kwa njia ya simu.
“Tafiti hizi zinaonesha bado kuna kundi kubwa la wananchi wanaofahamu huduma zisizo rasmi kama vikoba, lakini hawana uelewa wa huduma nyingine rasmi za kifedha,” amesema Mjema.
Ameeleza kuwa hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuweka mkakati wa kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kujikwamua kiuchumi.
“Mpango wetu ni kuona ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wamepata elimu ya fedha na kuweza kutumia huduma rasmi za kifedha,” ameongeza.
Mjema amesema maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka 2020/21–2029/30, ambapo elimu kwa umma ni kipaumbele kikubwa.
Amesema kupitia wiki hiyo, wananchi wa Tanga wanatarajiwa kupata uelewa mpana kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, kodi na dhamana za Serikali.
“Tunatarajia baada ya wiki hii, shughuli za kiuchumi ziongezeke, mapato ya halmashauri yaimarike na uwekezaji uongezeke, jambo litakaloboresha huduma za jamii kama elimu na miundombinu,” amesema.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Noves Mosea, amesema washiriki watanufaika kwa kujifunza namna ya kuwekeza kwenye dhamana za Serikali, kusimamia fedha binafsi na kuwasilisha malalamiko dhidi ya taasisi za fedha.
“Malalamiko yote kuhusu mikopo au huduma za kifedha yataelekezwa kupitia mifumo rasmi ikiwemo mfumo wa Sema wa Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Mosea.
Naye Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF, Linda Mshana, amesema mfuko huo umekuja na fursa mbalimbali za mikopo nafuu zitakazosaidia wananchi kuepuka mikopo ya kausha damu.
“Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata mikopo yenye riba nafuu na masharti rafiki ili kuboresha maisha yao,” amesema Mshana.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga na yatafunguliwa na Waziri wa Fedha, Balozi Hamis Mussa Omari, yakibeba kauli mbiu isemayo: “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi.