………
Na Mwandishi wetu – Zanzibar
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuongeza kasi katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji ambao wanaingia Zanzibar kwa shughuli za uwekezaji.
Ameyasema hayo Januari 19, 2026 alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za NIDA kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa, James Kaji Ikulu – Zanzibar.
Mhe. Rais amesema kuwa ameridhishwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na NIDA za kusajili na kutambua watu, ambapo zaidi ya asilima 94 ya Wazanzibari, wameshasajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa NIDA na kupata vitambulisho ambavyo wanaendelea kufurahia matumizi ya vitambulisho hivyo.
‘’Nawataka muongeze bidii ya kuwahudumia wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza hapa Zanzibar ili kuendana na kasi ya maendeleo katika uwekezaji, kwa kufanya hivyo, itarahisisha na kusaidia kukuza uchumi kwa haraka zaidi’’ Alisema Rais Mwinyi.
Kwa upande wake Mkugugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, James Kaji amesema kuwa Ofisi za NIDA zinaendelea vizuri na kazi ya usajili na utambuzi kwa wananchi wote wanaokidhi vigezo.
Ameongeza kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inatarajia kujenga ofisi za Usajili Visiwani Zanzibar katika Wilaya za Magharibi A, Micheweni na Kusini, pamoja na kufungua ofisi ndogo katika eneo la Tumbatu – Unguja na Kojani – Pemba ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuongeza kasi ya usajili.
Akihitimisha taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha NIDA kupata fedha kwa ajili ya kununua magari 145 ambayo kwa kiasi kikubwa yatarahisisha shughuli za usajili na utambuzi wa watu Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa Ushirikiano na kuiwezesha Ofisi ya Uratibu NIDA Zanzibari kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya msingi ya Usajili na Utambuzi Watu.


