LICHA ya dau zuri alilowekewa mezani na Yanga ili kuvaa jezi ya njano na kijani msimu huu, kipa wa Pamba Jiji, Yona Amos ameshindwa kujiunga na timu hiyo huku ikielezwa ameukwepa mziki wa Djigui Diarra.
Kipa huyo aliyebakiza miezi sita kuitumikia Pamba Jiji, alikuwa anawindwa na Simba na Yanga huku ofa ya Wanajangwani ikiwa ya kwanza kutua, lakini mambo yameenda tofauti na matarajio ya wengi baada ya Yanga kumtambulisha Hussein Masalanga akitokea Singida Black Stars.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga, kililiambia Mwanaspoti kilichowakwamisha kupata saini ya kipa huyo ni mwenyewe kuhitaji nafasi ya kucheza mara kwa mara kama ilivyo Pamba Jiji, kitu ambacho sio rahisi bila ya kupambania namba dhidi ya Diarra na Aboutwalib Mshery.
“Ni kweli tuliwekeza juhudi za kumpata kipa huyo na kuweka dau zuri mezani, lakini tumekwama katika kipengele cha kumhakikishia nafasi ya kucheza, kwani hilo linatokana na uwezo wake uwanja wa mazoezi akilishawishi benchi la ufundi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Yona amesema anaamini katika kukuza kipaji chake kwa kucheza kama ilivyo Pamba Jiji, hivyo ili aweze kutua katika kikosi chetu pia apate hiyo nafasi sio rahisi kwani timu tayari ina kipa namba moja na mbili, hivyo juhudi zake ndizo zingeshawishi benchi na sio sisi kumhakikishia.”
Kwa mujibu wa chanzo, Yanga ilimwekea Yona dau la Sh100 milioni na mkataba wa miaka miwili, lakini kitendo cha kutaka kucheza mara kwa mara, ikafanya dili hilo lishindikane.
Chanzo hicho kilipoulizwa ni kwa nini walimtaka kipa huyo wakati tayari wana makipa watatu Diarra, Mshery na Khomeiny Abubakar, kilisema Khomeiny anakaribia kumaliza mkataba lakini pia anasumbuliwa na majeraha.
“Tulikuwa tunapambana na Yona baada ya kubaini kipa wetu namba tatu ana majeraha na mkataba wake pia unamalizika, tulihitaji kipa atakayeongeza ushindani wa namba na kuongeza ubora wa makipa wengine,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga.
“Baada ya kukosa saini ya Yona akili kubwa ikatumika na kuamua kumalizana na Hussein Masalanga, tunaamini pia ni kipa sahihi kwa wakati huu,” kiliongeza.
Masalanga ametua Yanga kwa mkataba wa miezi sita akiwa ametoka kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 akiwa na Taifa Stars iliyoishia hatua ya 16 Bora kwa kutolewa na wenyeji Morocco waliopoteza mechi ya fainali juzi mbele ya Senegal.