Wanaodaiwa kusafirisha heroini, waendelea kusoka rumande

Dar es Salaam. Upelelezi kesi ya kusafirisha dawa za kulevya inayowakabili Abdallah Mwita (38)  na wenzake watatu haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Januari 19, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mwita na wenzake wanakabiliwa  na kesi ya uhujumu uchumi namba 5208 ya mwaka 2025, yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo heroini zenye uzito wa kilo 2.44

Mbali na Mwita ambaye ni mkazi wa Magomeni, washtakiwa wengine ni Abdallah Maggid(32) mkazi wa Survey, Said Alawy(40) mkazi wa Kariakoo na Halima Mwidini Nuru(23) mkazi wa Karikaoo.

Mwakamele ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo wakati kesi hiyo ilivyotajwa.

“Upelelezi wa kesi hii bado unaendelea, hivyo tunaomba tupangiwe tarehe nyingine” amesema Roida.

Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2026 kwa kutajwa.

Mshtakiwa Mwita, Maggid na Alawy wamerudishwa rumande kutokana kiasi cha dawa walichokutwa nacho hakina dhamana huku Halima akiwa nje kwa dhamana

Washtakiwa wanadaiwa kusafisha dawa hizo kinyume kifungu cha 15A(1) na (2) C cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la kwanza linawakabili Mwita, Maggid na Alawy, ni kusafirisha kilo mbili za heroini kinyume cha sheria.

Wanadaiwa Januari 16, 2025 eneo la Survey lililopo wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa Mwita, Maggid na Alawy walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 2.44, kinyume cha sheria.

Shtaka la pili ni kusafirisha mirungi, shtaka linalomkabili Alawy na Halima, ambapo wanadaiwa Januari 16, 2025 katika Mtaa wa Ukombozi uliopo eneo la Kariakoo, walikutwa wakisafirisha mirungi yenye uzito wa gramu 96.45.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao, Februari 28, 2025 mahakamani hapa.