Magata atambia rekodi mpya Mtibwa Sugar

KIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Fredrick Magata amesema kufunga bao katika mechi ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho msimu huu kwake ni rekodi mpya katika maisha yake, kwani hajawahi kufanya hivyo, tangu ameanza kucheza maishani.

Nyota huyo aliifungia Mtibwa Sugar bao la kusawazisha dakika ya 60, katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni na miamba hiyo ilishindwa kutambiana na kuisha kwa sare ya 1-1.

Akizungumza na Mwanaspoti, Magata amesema ni furaha kwake kufunga bao muhimu lililowapa pointi moja, ingawa siri kubwa ni kutokana na ushirikiano pia kutoka kwa benchi la ufundi na wachezaji wanaopambana kwa ajili ya timu hiyo msimu huu.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha haturudii makosa yaliyotokea nyuma kwa maana ya kuona timu inashuka tena daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship, hivyo, tutaendelea kupambana licha ya ushindani mkubwa uliopo,” amesema Magata.

Nyota huyo amesema siri ya kiwango kizuri kinachoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo ni kutokana na mafundisho mazuri ya benchi la ufundi la kikosi hicho linaloongozwa na Kocha, Mkenya Yusuf Chippo na msaidizi wake, Awadh Juma ‘Maniche’.

Licha ya kufunga bao hilo moja msimu huu, ila Magata anashikilia rekodi ya kupandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu kutokea Ligi ya Championship, baada ya kuanza akiwa na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025.

Msimu wa 2024-2025, Magata alichangia mabao 30 ya Mtibwa kati ya 58, baada ya kufunga tisa na kuasisti 21 na timu hiyo ilimaliza mabingwa na pointi 71, ikiungana na Mbeya City kurejea Ligi Kuu iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 68.