Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Moshi, imeruhusu kuendelea kwa kesi ya ardhi inayohusu mgogoro wa ardhi baina ya baadhi ya vijiji vinavyopakana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Aidha, Mahakama hiyo imetupilia mbali sehemu ya pingamizi la awali lililowasilishwa na wadaiwa likipinga uhalali wa kesi hiyo, kwa madai kuwa wadai waliwashtaki wahusika wasiostahili kisheria.
Mahakama ilikubaliana na hoja ya Serikali kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), hakuwa mshtakiwa sahihi kisheria, hivyo kuamuru jina lake lifutwe na badala yake TAA iongezwe kama mdaiwa katika kesi hiyo.
Mahakama hiyo ilikataa hoja ya upande wa Serikali kuhusu kufutwa kwa mshtakiwa wa nne, ikieleza suala hilo linahitaji ushahidi wa kina kuhusu hadhi ya majukumu ya Kampuni ya Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (Kadco), hivyo suala hilo haliwezi kuamuliwa kupitia pingamizi la awali.
Uamuzi huo umetolewa Januari 14, 2026 na Jaji Adrian Kilimi anayesikiliza kesi ya ardhi namba 30928/2024 iliyofunguliwa na wananchi 30 dhidi ya Mkurugenzi Mkuu TAA, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna wa Ardhi, Mkurugenzi Mkuu wa Kadco, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Wananchi hao 30 kutoka maeneo ya Sanya, Kijiji cha Mtakuja, Kijiji cha Tindigani vilivyopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo baada ya kusikiliza pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa wadaiwa.
Jaji baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, aliridhia sehemu ya pingamizi hilo la awali na kueleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA, hakuwa muhusika sahihi wa kushtakiwa na badala yake inashtakiwa Mamlaka ya TAA.
Hivyo Mahakama kwa kutumia mamlaka iliyopewa kisheria na kuamuru jina la Mkurugenzi Mkuu TAA lifutwe na badala yake TAA iongezwe kama mdaiwa.
Katika kesi hiyo, wadai hao wameshtaki taasisi na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakiomba Mahakama itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa ardhi wanayoishi kwa muda mrefu.
Walidai kuwa ardhi hiyo iliyovamiwa na Serikali bila ridhaa yao na walifanyiwa manyanyaso ya kimwili na kisaikolojia kutokana na jitihada za kuwaondoa katika maeneo hayo.
Miongoni mwa madai yao, wadai hao waliomba Mahakama itoe amri ya kuzuia kufukuzwa kwao katika ardhi hiyo, itamke kuwa hati miliki zilizotolewa kwa baadhi ya wadaiwa zilitolewa kinyume cha sheria na kuagiza kulipwa fidia kwa madhila yaliyowapata.
Baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo upande wa wadaiwa waliwasilisha notisi ya pingamizi la awali wakipinga uhalali wa kesi hiyo.
Hoja kuu ya pingamizi ilikuwa kuwa wadai waliwashtaki Mkurugenzi Mkuu wa TAA na Mkurugenzi Mkuu wa Kadco badala ya kuzishtaki taasisi huzika kama zinavyotambuliwa kisheria.
Wakili wa Serikali, Gloria Issangya, aliieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania namba 8 ya mwaka 2024, ni Mamlaka ya TAA pekee yenye uwezo wa kushtaki au kushtakiwa na siyo Mkurugenzi Mkuu.
Wakili huyo alisisitiza kuwa kuwataja viongozi hao binafsi kulifanya kesi hiyo kuwa batili kisheria na kuomba itupiliwe mbali kwa gharama.
Kwa upande wao wadai waliowakilishwa na Mawakili John Lairumbe na Joseph Melau, walipinga pingamizi hilo na kudai kuwa ni lazima lijikite katika hoja za kisheria bila kuhitaji ushahidi na kueleza hoja ya Serikali ilihitaji Mahakama kuchunguza ukweli na ushahidi kuhusu hadhi ya wadaiwa jambo lisiloruhusiwa katika pingamizi la awali.
Aidha, wanadai kuwa hata kama kulikuwa na dosari katika kuunganishwa, baadhi ya wadaiwa sheria inaruhusu Mahakama kurekebisha dosari hizo badala ya kutupilia mbali kesi nzima.
Jaji Kilimi amesema baada ya kuzingatia kwa makini hoja zilizotolewa na pande zote, anakubaliana na wakili wa wadai kwamba pingamizi la awali lililowasilishwa, linahitaji ushahidi ili kubaini kama kifungu tajwa kinatumika na kubaini kama mdaiwa wa kwanza na wa nne wanaangukia chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Amesema pingamizi la awali lina wajibu wa kuwa na msingi wa sheria ambayo inaweza kusuluhisha kesi bila kuhitaji kuthibitisha ukweli au kutoa ushahidi na kuwa katika jambo hilo limejikita katika Sheria ya Viwanja vya Ndege vya Tanzania namba 8/2024.
Jaji huyo amesema amesoma sheria hiyo iliyoidhinishwa na Rais Oktoba 2, 2024 na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la Oktoba 11,2024, hivyo amejiridhisha ni sheria halali na siyo muswada.
Amesema kwa mujibu wa Sheria hiyo, Mamlaka hiyo ina mamlaka ya kushtaki au kushtakiwa na hakuna mahali popote sheria hiyo imeeleza mamlaka hayo yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka.
Jaji amesema Mahakama imekubaliana na hoja ya pingamizi la awali kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA aliunganishwa isivyofaa kama mdaiwa.
Amesema badala ya kuitupilia mbali kesi nzima, Mahakama ilitumia mamlaka yake chini ya Amri ya 1 Kanuni ya 10(2) ya Kanuni za Utaratibu wa Madai na kuamuru kufutwa kwa jina la Mkurugenzi Mkuu wa TAA na badala yake jina TAA liongezwe kama mdaiwa.
Kuhusu mdaiwa wa nne (Mkurugenzi Mkuu wa Kadco), Mahakama ilisema kuwa suala la kama alipaswa kushtakiwa yeye binafsi au kampuni yenyewe linahitaji uchunguzi wa kina wa kisheria na wa kweli, jambo linalohitaji ushahidi.
Kwa msingi huo, Mahakama iliamua kuwa pingamizi la awali halikuwa na msingi kuhusiana na mshtakiwa huyo wa nne kwani halijajengwa kwa msingi wa sheria pekee.
“Katika hilo naona kwamba pingamizi la awali lina msingi kwa kiwango kilichopo hapo juu. Gharama zitakuwa katika kesi kuu,” amehitimisha Jaji akisema kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa baada ya uamuzi huo wa pingamizi la awali kutolewa.