Kihongosi: Viongozi wa halmashauri msiwe chanzo cha migogoro

Singida. Viongozi wa halmashauri nchini wameonywa kutokuwa chanzo cha migogoro ya wao kwa wao na badala yake watambue kazi yao ni kuwatumikia wananchi kwa nafasi zao bila kuwabagua.

Mbali na viongozi wa halmashauri, wasimamizi wa miradi wametakiwa kutanguliza utu kwa wafanyakazi ikiwemo kutowadhulumu stahiki zao na walipe kwa wakati kile walichokubaliana.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu Januari 19, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliojitokeza katika eneo la ujenzi wa mradi wa soko la kimataifa la vitunguu.

Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa (CCM) Kenani Kihongosi akisalimiana na wananchi wa Tarafa ya Ilongero leo Jumatatu, Januari 19, 2026 alipofika kutembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya a Ilongero.



Soko hilo limejengwa katika Kata ya Unyambwani, Kijiji cha Sekotule kilichopo katika Jimbo la Ilongero, mkoani Singida alipokagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.

“Viongozi wa halmashauri hakikisheni hamuanzishi migogoro katika maeneo yenu, angalieni mnaowatumikia ili muwahudumie kikamilifu bila kuwabagua, lugha zenu ziwe zenye ukarimu na kuwapa faraja wahitaji, lakini makandarasi angalieni haki za mnaofanya nao kazi, wapeni haki zao,” amesema Kihongosi.

Kihongosi amepokea taarifa za ujenzi wa mradi huo ambao ulianza Julai 7, 2025 na unatarajia kukamilika Oktoba 23, 2026 kupitia miradi ya Mradi wa Kubadilisha Miundombinu na Ushindani wa Miji Tanzania (Tactic).

Kwenye miradi hiyo, jumla ya Sh24.27 bilioni zitatumika kwenye ujenzi wa soko la kimataifa, ujenzi wa barabara za ndani na ujenzi wa mifereji wakati ujenzi wa hospitali ya halmashauri unagharimu Sh4 bilioni.

Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa (CCM) Kenani Kihongosi akizungumza na simu alipompigia Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa akimwomba kupeleka gari la wagonjwa katika hospitali ya Wilaya inayojengwa Ilongero



Kihongosi amemuagiza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kupeleka gari la wagonjwa katika tarafa ya Ilongero ambayo licha ya kujengwa Hospitali ya Wilaya, lakini hakuna gari hilo.

Mbunge wa Ilongero,  Haiderali Gulamali amesema wagonjwa wa maeneo hayo wanapata shida inapofika wanahitaji huduma za dharura.

Mwenyekiti wa soko hilo, Idd Mwanja amesema ujenzi huo unakwenda kumaliza changamoto na kilio cha muda mrefu cha kukosa masoko.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dengedo amesema soko hilo litakuwa kama sehemu ya kiwanda kwani panajengwa sehemu ya kuchakata zao la vitunguu vinapotoka shambani ili kuviweka kwenye ubora.