Chadema yasema ‘No Reforms, No election’ imekiimarisha chama

S: No Reforms, No Election ni kauli mbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), msingi wake ilikuwa ni kusukuma presha kwa dola na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwamba bila kufanyika mabadiliko ya Katiba na Sheria za Uchaguzi 2025 hakutakuwa na uchaguzi.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Said Mzee amesema kampeni ya ‘No Reforms, No Elections’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) imekiimarisha chama hicho.

Mzee amesema kampeni hiyo imeimarisha imani ya wananchi kwa chama hicho katika kipindi ambacho viongozi wake wamekumbwa na vifungo na vikwazo vya kisiasa.

No Reforms, No Election ni kauli mbiu ya Chadema, msingi wake ni kutaka mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi hasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwamba bila mabadiliko hayo kufanyika, uchaguzi usingefanyika.

Mzee ametoa kauli hiyo leo Januari 19, 2026 kupitia mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha) ukijikita kwenye historia ya Chadema upande wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 33 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Kwa mujibu wa Mzee, kampeni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Chadema kuendelea kuwepo na kuwa imara licha ya mazingira magumu ya kisiasa iliyopitia.

“Moja ya sababu Chadema kinaendelea kuwepo licha ya kuwekwa kifungoni ni hii kampeni. Watanzania wametuamini pasipo shaka kuwa tunasemea shida na mateso yao, ndiyo maana wakaibeba ajenda hii,” amesema.

Akizungumzia uanzishwaji wa kampeni hiyo, amesema viongozi wa chama walidhani wao ndio waliokuwa na uelewa mkubwa kuhusu changamoto za mfumo wa uchaguzi, lakini waligundua kuwa wananchi tayari walikuwa na uelewa mpana zaidi.

“Tulipoanza kampeni hii tulifahamu kuwa Watanzania walikuwa na uelewa mkubwa kuliko sisi. Matokeo yake ajenda hii ikahama kutoka kuwa ya Chadema na kuwa ya Watanzania wote,” amesema.

Akizungumzia suala la Katiba mpya, Makamu Mwenyekiti huyo amesema mabadiliko ya katiba yatafanikiwa kwa haraka endapo wazee na makundi ya kijamii yataungana bila kujali mgawanyo wao wa vyama vya siasa wala itikadi za kidini.

Kuhusu suala la maridhiano ya kisiasa, Mzee amesema hakuna dhamira ya kweli ya kufanikisha mchakato huo.

“Tumefungiwa kufanya siasa. Wanachama wawili wakikutana wanapewa kesi ya uhaini. Maridhiano hayawezekani katika hali hii,” amesema.

Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu ambaye angekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya maridhiano, yupo gerezani, hali inayofanya mchakato huo kuwa mgumu zaidi kwa chama hicho.

Pia, Mzee amezungumzia Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza matukio ya siku na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, akisema mwenendo wa baadhi ya watu wanaojitokeza kwenye Tume hiyo kukihukumu Chadema haumtishi bali kinachozungumzwa na watu aliowataja ni machawa ndicho kinampa wasiwasi.

“Tume imeundwa kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29, lakini kuna watu wanajitokeza kusema Chadema inahusika na hili au lile. Kwa nini wasiende kwenye Tume kutoa maoni yao badala ya kuita waandishi wa habari kuzungumza?” amehoji.