Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabiliwa washtakiwa 13 wakiwemo waliokuwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umekamilika.
Kwa sasa Jamhuri ipo katika hatua ya kusajili taarifa pamoja na nyaraka muhimu Mahakama Kuu ili washtakiwa hao wasomewe maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariagoreth Kunzugala, maarufu Bonge, Henry Mbowe maarufu kama Mzee wa Vichwa, Asha Sekiboko, Cecilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanaheri Omary, wote walikuwa wafanyakazi wa BoT na wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Wengine ambao sio watumishi wa BoT ni Alistides Genand, Mussa Chengula, Zaituni Chihipo na Respicius Rutabilwa.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwemo kuharibu noti Sh4.6 milioni kwa kuzichanachana na hivyo kuisababishia benki hiyo hasara ya zaidi ya Sh4.6 bilioni.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa.
Hakimu Mkazi Mkuu, anayesikiliza kesi hiyo, Anna Magutu aliipangia Januari 27, 2026 kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inadaiwa kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30, 2019, washtakiwa wakiwa watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Pia, inadaiwa Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makusudi, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga.
Katika shitaka la tatu, washitakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, walizikatakata noti za Sh460,000 na za Sh10,000 kila moja zenye thamani ya Sh4.6 bilioni.
Katika shitaka la nne, siku na maeneo hayo, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washitakiwa wote walijipatia faida ya Sh1.5 bilioni kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.
Katika shitaka la tano washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia BoT hasara ya Sh4.6 bilioni.
Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita, lakini Juni 18, 2021, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwafutia shitaka la kutakatisha fedha na hivyo kubaki na mashtaka matano.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba14, 2020.