Wazee walivyoongeza nguvu kuliponya Taifa

Dar es Salaam. Baada ya hatua zilizochukuliwa na makundi mbalimbali za kuliponya Taifa kutokana na maandamano na vurugu za Oktoba 29 mwaka jana, hatimaye wazee nao wamejitosa kuusaka mwafaka huo wa kitaifa.

Wazee wanakuja na uamuzi huo, wakati ambao tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda tume kuchunguza matukio hayo, ikipewa miezi mitatu kuifanya kazi hiyo, ingawa baadhi ya wananchi wamedai kukosa imani nayo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku mmoja wa wazee hao, amewasihi wananchi kuiamini tume kwa kuwa ina wajumbe wazoefu na kama kupinga wasubiri kuyapinga matokeo.

Hayo yote yanakuja, baada ya maandamano yaliyozaa vurugu siku ya uchaguzi Oktoba 29, mwaka jana na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu, uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.

Suala la wazee kujitosa kuusaka mwafaka wa kitaifa, limetangazwa leo, Jumatatu Januari 19, 2026 na Butiku alipozungumza na waandishi wa Habari, kuhusu kikao cha wazee kujadili vurugu hizo.

Katika mkutano wake huo, Butiku amesema kikao chao cha wazee kinalenga kujadili kwa kina imekuaje Taifa limefika katika hatua hiyo ya vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka jana.

“Umoja wetu ulitikiswa siku hiyo, haikuishia hapo, walioongoza tunaambiwa walikuwa ni vijana wetu, watoto ambao wanatoka katika matumbo yetu.

“Wana mambo na sisi wazee, wakapigana, wakapambana na polisi. Wakachoma nyumba na nini na nini na Dar es Salaam ninyi mlikuwepo mliamrishwa mkae ndani watu zaidi ya milioni tano,” amesema.

Amesema kuna simulizi zinazodai kwamba waliotoka nje siku hiyo kwenda kununua mahitaji, walipigwa risasi.

“Mimi naamini katika utawala wa kijeshijeshi amri ukiipuuza kama kweli polisi waliona hatari ya kuchoma bandari na majengo mengine, unaweza kusema kama ni polisi hivi, haya kaeni ndani, sitetei lakini nasema kilichotokea,” amesema.

Katika mazungumzo yake hayo, Butiku amesema wazee wanaona kwa yaliyotokea Oktoba 29, ni uthibitisho kuwa Taifa limeanza kushindwa katika utawala wa sheria.

“Vijana wetu wamelazimika kwenda mtaani. Nchi imeanza kushindwa kwa hiyo leo hali ikoje. Tunakutana hapa kuzungumza hali halisi ya Taifa letu, tumefikaje katika msiba huu,” amesema Butiku.

Amesema kikao hicho cha wazee kinalenga kutafuta ukweli, kwa sababu wanaona Taifa limeanza kushindwa kuishi katika mfumo wa sheria.

Amesema Katiba imebainisha wazi kuwa Mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa uhai wa mtu tena kwa utaratibu wa kisheria.

Amesema haiwezekani kuwa na nchi ambayo raia wanapotea, wanaburutwa wanapotelea vichakani.

Sambamba na hayo, Butiku amesisitiza kutokana na yanayoendelea nchini na kile kilichotokea Oktoba 29, mwaka 2025, wazee wameona wafanye kikao kuujadili ukweli na kutafuta mwafaka.

Katika mazungumzo hayo, Butiku amewasihi Watanzania kuikubali tume iliyoundwa na Rais Samia kuchunguza vurugu hizo, akisisitiza kama kukataa, wasubiri wayakatae matokeo.

“Imeundwa tume, sasa tume hii ina ubishi, oooh… tume gani, watu waliomo, hatuwaamini, hili ni tatizo, sasa kama hatuwaamini kuna majaji wawili pale, watu wetu wakubwa kabisa.

“Mimi naomba tuikubali, lakini ndiyo Tume ya Rais, aliyoichagua, chombo cha kutuletea taarifa, yale yatakayokuwepo tunayakubali sawa, tuje tuyakatae sawa… lakini tusikatae tume, tuiunge mkono ituletee habari,” amesema.

Akizungumzia suala la katiba mpya, Butiku amesema changamoto nyingi za utawala wa sheria zinazoshuhudiwa, msingi wake ni Katiba ambayo kwa kipindi kirefu imeshindikana kufanyiwa mabadiliko.

Lakini, amesema kuna matumaini ya hilo kutokea hasa baada ya mkuu wa nchi wa sasa (Rais Samia), kuahidi kuanza kulifanyia kazi hilo ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.

Afichua mazungumzo yake na Polepole

Butiku amesema kabla ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alikutana naye mara mbili kwa mazungumzo naye.

Kauli hiyo ya Butiku, inakuja ikiwa ni miezi mitatu tangu Polepole, alipochukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake eneo la Ununio, Dar es Salaam usiku wa Oktoba 6, 2025, tukio lililotokea miezi minne baada ya kujiuzulu ubalozi wa Cuba na kuanza kuikosoa Serikali na viongozi wake.

Baadaye Agosti 5, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wa Polepole na kumvua hadhi ya ubalozi.

Hata hivyo, Polepole mwenyewe katika moja ya video zake baada ya kujiuzulu amewahi kueleza kuwa kabla hajajiuzulu, alikutana na wazee kadhaa kuwaeleza changamoto zake na kuwaomba ushauri, ingawa hakuwataja majina.

Butiku amesema mara ya kwanza, Polepole alimfuata na kumweleza changamoto zake za kazi alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kabla hajahamishiwa Cuba.

“Mara ya pili akaja anasema kusiwe na uchaguzi, nikamwambia kama hakuna uchaguzi hamtakuwa na Rais, kama huna Rais nani ataongoza nchi yenu, hatukukubaliana akaenda,” amesema.

Mara ya tatu, amesema hawakukutana bali alimpigia simu na kumweleza kwamba, kama ajenda ya kutofanyika uchaguzi haitakuwepo, anaona bora aache kazi (ya ubalozi wa Cuba).

“Nikamjibu fuata dhamiri yako. Asiniombe ruhusa kama anataka kuacha kazi, mimi sikumchagua, fuata dhamira yako, tangu wakati huo nilichomuona ni kwamba yuko kwenye mitandao, mwisho nimeona damu yake ni hii lakini mwenyewe sikumwona, mnajua aliko?” amehoji.

Hata hivyo, Butiku amesema ameona katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu wanadai anafahamu alipo Polepole, akisema hajui chochote, huku akilaani kitendo cha kutoweka kwake.

“Wako wengi (waliopotea), mmoja kijana mwenzenu Polepole (Humphrey) wanamtafuta mnajua aliko? Wanasema mimi najua, nataka kuwaambia leo sijui,” amesema Butiku.

Butiku amesema nyumba yake ni miongoni mwa zilizopangwa kuchomwa moto akisema alipewa taarifa kuwa waandamanaji wanakwenda kwake, huku akiwa ndani.

“Wengine tuliletewa taarifa mimi ni mmoja wao, niliambiwa tunakuja kuchoma moto nyumba yako, iko mkoani Mara, nikasema mimi sijatoka nyumbani kwangu, vijana hawa wakanikuta, wakanibembeleza weee… watu wa usalama.

“Niliwauliza mnataka kunipeleka wapi, wakasema kwenda kukuficha na nani na wengine VIP, nikajiuliza kina nani Mkoa wa Mara huu, nikakataa waende kunificha labda hao wanaonificha nao ndio wananimaliza, nikawaambia huko siendi,” amesimulia Butiku.

Amesema aliwaambia atajificha mwenyewe na hakumwambia nduguye yeyote alikokwenda kwa kuwa aliambiwa nyumba yake itachomwa moto.

“Bunda (mkoani Mara) pale Ofisi ya TRA ilichomwa, nyumba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira imechomwa, nchi ikajaa askari polisi, kutishanatishana hivyo, uoga ukaingia, wakatoka TPDF kusaidia, wakabaki peke yao,” amesema.