Dar es Salaam. Bado msimamo wa chama cha ACT-Wazalendo kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) umeendelea kuwa mwembamba, baada ya chama hicho kusema si kipaumbele chake kwa sasa.
Kimesema kinatathmini kuona iwapo malengo ya kuundwa kwa SUK yanatimizwa kwa mfumo uliopo na kama hayatimizwi, hakitaona haja ya kuingia ndani ya Serikali hiyo, bali itawaachia wananchi waamue.
Hata hivyo, chama hicho kimesema jukumu la kuifanya tathmini hiyo limeachwa kwa kamati maalumu iliyoundwa na kubarikiwa na Kamati Kuu, ili kubaini kama malengo ya kuanzishwa kwa serikali hiyo yanatimizwa au vinginevyo.
ACT-Wazalendo inakuja na msimamo huo wakati zimebaki siku 21 kati ya zile 90 ambazo, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kinapaswa kiwe kimeingia SUK kwa kuwa kilipata zaidi ya asilimia 10 ya kura za urais.
Jana, kupitia kikao chake cha Kamati Kuu, ilitarajiwa kuwa siku ya chama hicho kutoka na uamuzi wa mwisho kuhusu kuingia au kutoingia katika serikali hiyo, lakini bado haujaeleweka.
Msimamo huo wa ACT-Wazalendo umetolewa jana, Jumatatu Januari 19, 2026, na Makamu Mwenyekiti wake, Issihaka Mchinjita, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu.
Mchinjita amesema kwa sasa kipaumbele chao si kujiunga na SUK, bali ni kutathmini malengo ya kuundwa kwa serikali hiyo kama bado yanatekelezeka kwa mfumo uliopo.
Amesisitiza endapo malengo ya SUK hayatofikiwa kwa uelekeo uliopo, hawataona sababu ya kuingia katika serikali na badala yake watawaachia wananchi waamue mustakabali wao.
Kiongozi huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani kwa upande wa Zanzibar amesema SUK haikuundwa kwa lengo la kupora mamlaka ya wananchi ya kuchagua viongozi wao.
Amesisitiza uhalali wa Serikali unatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki unaowawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, akidokeza kuwa katika uchaguzi uliopita haijulikani nani alishinda.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikuwa kichaka cha kuiba kura, mwizi akaingia madarakani, halafu aliyeshindwa aitwe ili wagawane madaraka, kisha mchakato huo urudiwe tena,” amesema Mchinjita.
Kabla ya kuundwa kwa SUK, amesema damu za wananchi zilimwagika na wengine waliuawa, hali iliyolazimu kutafutwa suluhu ya kudumu ya migogoro ya kisiasa iliyokuwa ikijirudia kila baada ya miaka mitano.
Amesema SUK ilikusudiwa kuwa chombo cha kuwaleta Wazanzibari pamoja, kutatua changamoto zao za ndani na kuongoza nchi kwa mshikamano, hata hivyo jaribio hilo limeshindwa katika chaguzi zilizopita.
Mchinjita ameeleza ACT-Wazalendo haiwezi kujadili kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa bila kuanza na misingi ya kuundwa kwake, akisisitiza Serikali halali lazima itokane na uchaguzi halali unaotoa matokeo yanayoeleweka.
“Ni lazima kuwe na uchaguzi unaoeleza wazi nani ni Rais na nani amepata kura za kutosha kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tatizo hilo lazima lishughulikiwe kwanza,” amesema.
Ameongeza kuwa chama hicho kinajitenga na mjadala unaoendeshwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kama ACT-Wazalendo wataingia au la katika serikali hiyo.
“Huo si mjadala wetu. Sisi tunataka kujadili malengo ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kama malengo hayo hayawezi kufikiwa kwa mtindo unaoendelea sasa, basi haina haja ya serikali hiyo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo imeunda timu maalumu ya kushughulikia suala hilo, ikisisitiza kuwa mjadala mkubwa si kuingia au kutokuingia serikalini, bali ni misingi ya kuwepo kwa SUK.
Mchinjita amesema chama hicho kimegomea kuwasilisha jina la Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, licha ya taratibu kutaka jina hilo liwasilishwe ndani ya siku saba.
“Tulieleza kuwa hatuoni uchaguzi unaobainisha nani ni Rais na nani anastahili kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Msimamo wetu kwa sasa hatupo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema.
Amesisitiza kuwa dhamira ya ACT-Wazalendo ni kurejesha haki ya Wazanzibari ya kuamua kwa uhuru aina ya serikali wanayoitaka, huku akibainisha kuwa kamati iliyoundwa imepewa baraka na Kamati Kuu kupigania haki hiyo.
Akizungumzia hilo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo kwa upande wa Zanzibar, Khamis Mbeto, amesema kuwepo kwa SUK si takwa la chama fulani.
Amesema SUK ni takwa la Katiba ya Zanzibar na ACT-Wazalendo na viongozi wake wanafahamu kwa kina kuwa hilo ni jambo la kikatiba.
Mbeto amesema haieleweki kwa nini ACT-Wazalendo inadai aliyeshinda hafahamiki, ikiwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza matokeo na wameyasikia.
“Kila kitu, hasa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, ZEC imefanya vema. Wao (ACT-Wazalendo) wanapata wapi nguvu ya kudai hawaelewi wakati walisaini fomu za maadili?” amehoji.
Amesema chama hicho kilikuwa na mawakala katika maeneo yote na walisaini fomu za matokeo za kila kituo, hivyo haieleweki kwa nini wanadai hawaelewi mshindi.
“Wanatafuta huruma ya wananchi waliowaaminisha vibaya. Sisi hilo halitusumbui,” amesema Mbeto.
Amesisitiza kuwa wasipojiunga katika SUK, Serikali itaendelea na itawatumikia wananchi kwa sababu hicho ndicho kipaumbele cha CCM.
“Kipindi cha Dk Shein (Ali Mohamed, Rais wa sita wa Zanzibar), walisusa kuingia SUK, lakini Serikali iliendelea na wananchi walitumikiwa hadi Dk Shein alipomaliza kipindi chake. Kwa hiyo, hakuna kitakachokwama,” amesema.
Amesema wanachosubiri ni siku 90 zifike ili waunde Serikali, na mambo yataendelea kama ilivyokuwa enzi za Dk Shein.