Chukua hatua hizi unapokuta mwili wa binadamu barabarani, kichakani

Dar es Salaam. Fikiria unaamka asubuhi kuelekea kwenye shughuli zako, ghafla anakutana na mwili wa mtu aliyelala kando ya barabara au kichakani, hofu, taharuki na maswali huanza je, mtu huyu amekufa, nimsaidie, nimpe taarifa nani? au nikimbie?.

Hayo ni miongoni mwa maswali na sitofahamu za baadhi ya wananchi katika hoja ya swali kwamba, utafanya nini, ukikuta mwili wa mtu anayedhaniwa amekufa ukiwa barabarani au kichakani?.

Majibu ya wengi katika swali hilo yamedhihirisha uelewa mdogo wa jamii kuhusu hatua sahihi za kuchukua wanapokutana na tukio la namna hiyo.

Kati ya majibu 281 yaliyotolewa kwenye mtandao wa Mwananchi wa Instagram Oficial, zaidi ya nusu walieleza hatua pekee watakayoichukua ni kukimbia na kutotoa taarifa kokote, wakihofia kuhusishwa kama shahidi namba moja na kusaidia upelelezi.

Kupitia mtandao wa instagram wa Mwananchi official, mwenye akaunti ya jitu_la_mungu12 yeye amesema atakachokifanya ni kukimbia na kutokomea akiamini kwamba kwa sheria za Tanzania zilivyo ataambiwa aisaidie polisi.

“Unaweza kujikuta unapewa kesi, mpaka ije kujulikana sio wewe ulishakaa mahabusu muda mrefu, cha kujiuliza polisi wamesomeshwa kujua kupeleleza, lakini utaambiwa wewe uwasaidie, katika hilo ni kukimbia tu ili kujiepusha na mengine,” amesema.

Mwenye akaunti ya ferm.adezedward amesema hawezi kusaidia kutoa taarifa akieleza alivyowahi kumsaidia dereva bodaboda aliyegongwa.

“Nilijilaumu kwa nini nilitoa msaada, mambo yalikuwa mengi na kibaya zaidi polisi wengi wa Tanzania wanawaza kutumia nguvu,  ikitokea hivyo hatua pekee ni kupita mbali kukwepa ushahidi,” amesema.

Wakati mwenye akaunti ya emback12 amesema ukitoa taarifa si ajabu kujikuta polisi wa Tanzania wanakubadilisha ratiba zako zote na kila kinachokuhusu kikasimama na kuwa mtu wa kuripoti polisi.

“Utaanza kuulizwa hadi huyo mtu amekufaje wakati na wewe ulimkuta tu barabarani na si ajabu kama kauwawa basi hawamtafuti muuaji na kukutaka wewe (uliyesaidia kutoa taarifa) umtafute na kumleta muuaji,” amesema.

Mwenye akaunti ya pamhaytham amesema hawezi kuchukua hatua yoyote zaidi ya kupita mbali na kuondoka akihofu kuulizwa huko kichakani hadi kukuta mwili alikwenda kufanya nini?.

Wakati mwenye akaunti ya jimmy_joyouz akieleza namna alivyowahi kusaidia kubeba majeruhi aliyegongwa na boda kisha aliyemgonga akakimbia.

“Tulikwenda polisi wakatupa pf3 ili nimpeleke hospitali, na kutakiwa kumsimamia nikajua atatibiwa bure, kilichonikuta nilipoteza muda, fedha na nguvu, hapo ni majeruhi je, kwa maiti si ndiyo utaambiwa uchimbe kaburi mwenyewe, binafsi nitapita mbali,” amesema.

Mwenye akaunti ya Jojumo_nanack_mmary amesema atakimbia zaidi ya marathoni akiamini msaada wa kutoa taarifa utageuka hukumu na lawama kwake.

“Ukitoa taarifa bado utawekewa walakini na polisi, si ajabu hata jamii na familia ya mlengwa watahisi ni wewe ndiye umefanya tukio hilo, bora kupita mbali,” amesema.

Akizungumzia kwa muktadha wa kisheria, wakili Hekima Mwasipu amesema unapokutana na tukio la aina hiyo, jukumu lako ni kutoa taarifa kwenye mamlaka husika basi.

“Hakuna sheria inayosema wewe mtoa taarifa ndiye utakuwa shahidi namba moja, sheria inasema kila raia ana wajibu kuripoti tukio lolote la kijamii, hivyo hata katika hili jukumu lako ni kuripoti tu polisi au kwa mjumbe au mwenyekiti wa mtaa,” amesema.

“Mtu anapofariki tafsiri yake amefariki kifo cha asili au amefanyiwa ukatili, haijalishi amekufaje, ukikuta mwili barabarani au kichakani wajibu wako ni kutoa taarifa tu kwenye mamlaka husika.

“Jeshi la Polisi ndilo lina mamlaka kufanya uchunguzi wa mwili uliokufa kitatanishi, kama polisi wako mbali basi unatoa taarifa kwenye mamlaka za eneo husika, hususani vijijini unatoa taarifa kwenye mamlaka za kijij,” amesema.

Amesema uongozi wa kijiji ndiyo utakuwa na jukumu la kutoa taarifa polisi na mtu mwingine hapaswi kuugusa huo mwili zaidi ya polisi.

“Hofu kwamba ukitoa taarifa wewe ndiye utasaidia polisi katika upelelezi si kweli, unachotakiwa ni kutougusa kabisa na baada ya kutoa taarifa kwenye mamlaka husika jukumu lako linaishia hapo,” amesema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime  leo Januari 19, 2026 alipoulizwa na Mwananchi juu ya hatua zipi mtu achukue amesema watu ambao wamewahi kuona au kushuhudia matukio kama hayo bila woga wanapaswa kutoa taarifa polisi au kwa viongozi wa serikali za mitaa.

Amesema wapo wanaotoa taarifa kwa watu wengine wanaowaamini nao wakatoa taarifa polisi.

“Pamoja na kutoa taarifa wanachukua hatua za kulinda eneo hilo hadi askari Polisi wanapofika na kufanya uchunguzi jambo ambalo linasaidia kulinda ushahidi.

“Hivyo basi pale mtu yeyote anapoona au ameshuhudia mwili wa mtu anayedhaniwa amefariki hana sababu za kuogopa bali anachotakiwa kufanya ni kutoa taarifa polisi kupitia namba 112 au 0699 998899.

“Akiona hawezi kufanya hivyo atoe taarifa kwa uongozi wa serikali za mitaa au kwa mtu mwingine yeyote yule anayemwamini.

Amesema wananchi wafahamu kuwa eneo la tukio kama hilo ni vizuri kulilinda ili lisiharibiwe na itasaidia kulinda ushahidi ambao utapatikana baada ya uchunguzi wa kisayansi.

“Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi tusijengeane hofu ambayo haipo kwani kuna matukio tena mengi yalishashuhudiwa, walioona wakatoa taarifa na wapo salama hadi leo kwani wao ni watoa taarifa na siyo waliofanya au waliotenda tukio hilo,” amesema.

Wenyeviti serikali za mitaa wafunguka

Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa wamesema inachotakiwa cha kwanza ni kutoa taarifa polisi.

“Wapo ambao wakiona wanaogopa kutoa taarifa polisi, ndipo wanakuja serikali ya mtaa, lakini hata huyo mtu akiwapigia simu polisi kutoa taarifa wanakuja,” amesema Mwenyekiti wa Mtaa wa Kumba Kibaha, Frank Msimbe.

Mwenyekiti mwingine wa mtaa Tangamano, Tabora, Juma Nassib amesema sio kweli kwamba anayetoa taarifa polisi ndiye anasaidia upelelezi.

‘Ingekuwa ni hivyo basi miili inayokutwa imekufa barabarani au kichakani ingekuwa inaozea huko, maana wengi wangeogopa kutoa taarifa, unapokutana na tukio la namna hiyo ni kutoa tu taarifa na polisi wakija wanathibitisha,” amesema.

Amesema ambacho polisi watakihitaji ni mahojiano ya mara kwa mara na wewe uliyetoa taarifa na si vinginevyo,” amesema.