WINGA wa Azam FC, Tepsi Evance ametua JKT Tanzania kwa mkopo wa miezi sita akiungana na aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Sospeter Bajana ambaye alitua kikosini hapo mwanzoni mwa msimu huu.
Tepsi ambaye alirudi Azam FC mwanzoni mwa msimu huu akitokea KMC ambayo alikuwa anaichezea kwa mkopo, amehudumu Azam FC kwa miezi sita na kutolewa tena kwa mkopo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Azam FC, kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wamemtoa mchezaji huyo kwa mkopo baada ya mapendekezo ya benchi la ufundi na wanaamini ni sehemu sahihi waliyompeleka mchezaji huyo kuendelea kukuza kipaji chake.
“Tepsi atakuwa JKT Tanzania hadi mwisho wa msimu, ni mkopo wa miezi sita, tunaamini tumempeleka sehemu sahihi ili aweze kupata muda wa kucheza, hivyo ni juhudi zake kwenye uwanja wa mazoezi.
“Benchi la ufundi licha ya kuonyesha kuwa na uhitaji wa kusajili wachezaji wa kuongeza nguvu kikosini, pia ilihitaji kupunguza idadi ya wachezaji ili kupishana na wanaoingia, Tepsi ni miongoni mwao,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema miezi sita ya winga huyo ndani ya JKT Tanzania, itathibitisha hatma yake ya kuendelea kubaki Azam au kutafuta timu nyingine kwani mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu baada ya kuongezwa mwaka mmoja mwanzoni mwa msimu.
Winga huyo ameitumikia Azam FC tangu Mwaka 2019 alipopandishwa timu ya wakubwa na kocha Etienne Ndayiragije na baadaye kutolewa kwa mkopo kwenda Ihefu ya Mbalali mkoani Mbeya ambayo sasa inajulikana kwa jina la Singida Black Stars baada ya kuuzwa.