KIKOSI cha Yanga jana jioni kilikuwa uwanjani kumalizana na Mashujaa kabla ya kuanza safari ya kwenda Misri kuvaana na Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Ijumaa wiki hii, jijini Alexandrea kabla ya kurudiana nao Januari 30, 2026 visiwani Zanzibar.
Pambano la jana lilikuwa la kwanza kwa Yanga katika Ligi Kuu kwa mwaka huu wa 2026, lakini kuna ubora fulani wa ukuta wao utasumbua kama timu zingine hazitajipanga sawasawa.
Kwanza imetokea katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwa Yanga kulibeba taji hilo bila kuruhusu bao lolote nyavuni mwao ikiwa ndio timu bora yenye safu bora ya ulinzi.
Katika Ligi (kabla ya jana) Yanga ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache ambalo ni moja katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya KMC, Novemba 9,2025 na hadi ligi hiyo iliposimama Desemba 7, 2025, ilikuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 16 na kufunga mabao 12.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves hatakuwa na presha kwani katika kikosi chake ana seti mbili bora za ukuta wake ambao jeuri itakuwa kwake amtumie nani na hii inampa jeuri kukabiliana na timu yoyote katika mechi za Ligi Kuu na hata ile ya kimataifa.
Katika michuano ya kimataifa, mechi mbili ilizocheza haijaruhusu bao lolote, kwani ilishinda 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco kisha ikatoka 0-0 na JS Kabylie ya Algeria, ikiwa ndiyo timu pekee kati ya nne katika hatua ya makundi ya CAF msimu huu ambayo haijaruhusu bao.
Simba inayoshiriki pia Ligi ya Mabingwa, yenyewe imeruhusu mabao matatu hadi sasa ikipoteza 1-0 kwa Petro Atletico ya Angola kisha kulala 2-1 mbele ya Stade Malien ya Mali, wakati Azam iliyopo Kombe la Shirikisho Afrika imeruhusu mabao matatu bila kufunga bao, huku Singida Black Stars yenyewe ikifungwa mabao matatu pia na kufunga bao moja.
Ukuta wa Yanga unaweza kumfanya kocha Pedro Goncalves kuamua aanze na majembe yapi katika mechi moja na ikishuka tena kwa pambano jingine kupanga watu wengine na wala usione tofauti yoyote, kulingana na matokeo ya mechi aliyofanya mabadiliko katika eneo hilo la ulinzi.
Pedro anaweza kuwa na ukuta huu kwenye seti yake ya kwanza, akianza na kipa Djigui Diarra, beki wa kulia Israel Mwenda, kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wakati mabeki wakati wakiwa Dickson Job na Ibrahim ‘Bacca’ ambaye jana alimalizia adhabu yake ya kusimamishwa mechi tano kwa kosa alililofanya katika mechi dhidi ya Mbeya City.
Ukuta huo una watu wote bora wanaoweza kuhimili presha yoyote na Pedro anaweza kushusha presha akiwatumia mabeki hao na kuipa timu hiyo utulivu mkubwa.
Rekodi zikionyesha katika mechi za Ligi Kuu ukiondoa zile ambazo Bacca alikosekana, bado Yanga iliruhusu bao moja katika mechi sita zilizopita (kabla ya jana) na kwa mechi za kimataifa ilifungwa bao moja tu ilipolala ugenini mbele ya Silver Strikers ya Malawi.
Aidha Pedro anaweza kuamua kutoka kivingine akianza na kipa Aboutwalib Mshery, beki wa kulia Yao Kouassi ambaye anaendelea kuimarika taratibu akitokea kwenye kukabiliana na majeraha ya muda mrefu. Pia kuna Kibwana Shomary aliyemtumia katika Kombe la Mapinduzi 2026.
Kule kushoto anaweza kuanza Chadrack Boka, mabeki wa kati wakiwa nahodha Bakari Mwamnyeto ambaye amethibitisha kiwango ni kitu cha muda lakini ubora ni wa kudumu baada ya kuonyesha ubora mkubwa akiwa kwenye Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2025 ambaye hapa atacheza sambamba na Mghana, Frank Assinki.
Ukuta huo kwa sehemu kubwa ndio uliotumika katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kabla ya Fainali kuongezwa kwa Job na Bacca na timu hiyo haikuruhusu bao lolote kwa dakika 90 za kawaida na hata zile za nyongeza 30 kama ilivyokuwa katika fainali dhidi ya Azam FC.
Kumbuka Yanga imemuongeza kipa Hussein Masalanga aliyekuwa Singida Black Stars aliyeng’ara katika fainali za AFCON 2025 akiwa na Taifa Stars akidaka mechi mbili dhidi ya Tunisia na Morocco, pia kuna beki wa kati Nizar Abubakar ‘Ninju’ aliyetumika pia katika Kombe la Mapinduzi 2026.
Kocha Pedro akizungumzia ubora wa Mwamnyeto, amesema beki huyo ni moja ya wachezaji bora waliopo kwenye kikosi chake ambapo sasa anaamini ataongeza upana wa machaguo kwa mabeki wanne alioano.
Aliongeza kuwa, mabeki wote alioano ni bora ambapo sasa wataimarisha ushindani wa nafasi na kuongezea ubora timu yao kwenye mechi zake huku akiahidi kuwapa nafasi kila mmoja.
“Ni kweli nimemuona Mwamnyeto, alikuwa kwenye kiwango bora kwenye fainali za Afcon, amethibitisha ni kiongozi sahihi kwa wenzake, kwetu ilikuwa furaha kuona wachezaji wetu wameimarika, Bacca pia, Job na Hussein nao walifanya vizuri.
“Kwetu hii ni nzuri, unaona sasa kama ambavyo unasema tuna upana wa kuchagua nani tumpe mechi ipi kutokana na ubora wa kila mchezaji, watakapokuwa wanashindana kuwania nafasi hapo ndio timu itanufaika kwa kuwa wote ni bora.
“Kila mchezaji ana nafasi ya kuitumikia timu, tunarudi kwenye ligi, kwa ratiba ilivyo tutakuwa na mechi za karibu sana, tuna mechi za Ligi ya Mabingwa, pia tutakuwa na mashindano ya FA, kumbuka tunatoka kwenye Kombe la Mapinduzi, tulikuwa na ratiba ngumu kidogo, ni lazima tuwe na akili ya kufanya rotesheni ili tutunze viwango vya wachezaji wetu,” amesema.