Pamba Jiji yang’oa kitasa Mbeya City

UONGOZI wa Pamba Jiji umemalizana na aliyekuwa beki wa kati wa Mbeya City, Gabriel Mwaipola ambaye anaenda kuziba pengo la Abdallah Kheri ‘Sebo’ aliyetimkia Singida Black Stars.

Pamba Jiji imekamilisha usajili wa beki huyo akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo ya jijini Mbeya iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu, ikizipiku Dodoma Jiji na TRA United ambazo pia zilikuwa zinawania saini ya kitasa hicho.

Chanzo cha kuaminika kutoka Pamba Jiji kililiambia Mwanaspoti, walipata saini ya beki huyo ambaye ni pendekezo la kocha Francis Baraza aliyesisitiza kuongeza mchezaji eneo hilo.

“Haikuwa rahisi kumpata nguvu ya Fedha imetumika kwani mchezaji alikuwa na ofa nyingi mezani tumefurahi kufanikisha usajili wake kwani ni mchezaji ambaye kocha ameonyesha kumkubali na anaamini ni mbadala sahihi wa Sebo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kwa mujibu wa ripoti ya kocha sehemu muhimu ambayo ilitakiwa kuongeza nguvu ni hiyo ya beki wa kati ambayo tayari tumeikamilisha, nafikiri hakuna haja ya kujaza wachezaji wengi kwani kocha amependekeza eneo ambalo ameona kuna mapungufu.”

Alipotafutwa kocha Baraza amesema uongozi umemthibitishia kukamilisha usajili eneo ambalo nilisisitiza lifanyiwe kazi kinachosubiriwa ni utambulisho wa mchezaji huyo.

“Juu ya usajili nilisema hapo awali kuwa hatutakuwa na mabadiliko mengi kwa sababu wachezaji wote wapo kwa hali nzuri hivyo sijaona haja ya kuongeza wachezaji wengine zaidi ya eneo la beki wa kati ambaye tayari ameshasajiliwa,” amesema

Baraza aliyeiongoza Pamba Jiji kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kukusanya pointi 16 baada ya mechi tisa, ikishinda nne na kutoka sare nne huku ikipoteza pambano moja mbele ya Yanga.