Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei amefariki dunia usiku wa kuamkia Januari 19 2026 akiwa na umri wa miaka 94.
Kwa mujibu wa taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche aliyoichapisha katika ukurasa wake, Mzee Mtei amefariki dunia akiwa mkoani Arusha.
“Tunachukua nafasi hii kutoa pole sana kwa familia ya Mzee Mtei, ndugu, jamaa na marafiki.
CHADEMA imepoteza moja ya nguzo imara sana za chama chetu.
Tutamuenzi Mzee Mtei kwa mema yote aliyoyafanya kwa chama na nchi yetu.
Pumzika kwa amani mzee Mtei.
Katika ukurasa huo wa Heche, taarifa hiyo inaeleza kuwa mipango ya mazishi inaendelea nyumbani kwa mzee Mtei eneo la Tengeru jijini Arusha.

Edwin Mtei, kabla ya kuanzisha CHADEMA, pia aliwahi kuwa Waziri wa zamani wa fedha.
Aidha, Heche amesema CHADEMA kitatoa taarifa rasmi kuhusu mwasisi huyo leo.
Mwanaharakati na Mkurugenzi wa Taasisi ya GH Foundation, Godlisten Malisa, naye ameandika katika ukurasa wake: “Tunamshukuru Mungu kwa maisha yake na mchango wake mkubwa katika Taifa hili. Tumuombee pumziko la amani na kuiombea faraja familia.”
Related
