Wanafunzi 14 wafariki ajalini, Rais Ramaphosa atuma rambirambi

Afrika Kusini. Wanafunzi 13 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi dogo la lori nje kidogo ya Jiji la Johannesburg na mwingine mmoja amepoteza maisha wakati akipatiwa matibabu hospitali.

Kutokana na ajali hiyo, Rais Cyril Ramaphosa ametuma salamu za rambirambi na ametoa wito polisi kusimamia utekelezaji wa sheria za usalama barabarani na kuboreshwa kwa usimamizi wa huduma za usafiri wa wanafunzi ili kuwalinda wanafunzi

Taarifa ya Polisi imesema iliyotolewa jana Jumatatu asubuhi Januari 19, 2026, imeeleza kuwa basi dogo lililokuwa limewabeba wanafunzi liligongana uso kwa uso na lori karibu na mji wa viwanda wa Vanderbijlpark, takribani kilomita 60 kutoka Johannesburg.

Uchunguzi wa awali wa Polisi umebainisha kuwa dereva wa basi la wanafunzi alishindwa kulidhibiti gari na kuchukua tahadhari wakati alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine.

Wanafunzi wengine kadhaa bado wako  hospitalini wakipatiwa matibabu. Polisi imesema wanafunzi waliokuwemo kwenye basi hilo dogo walikuwa ni shule za msingi na sekondari, baadhi yao wakiwa na wa miaka sita.

Picha za mitandaoni zimeonyesha basi hilo likiwa limeharibika kando ya barabara, huku wazazi wakiwa wamekusanyika kutambua miili ya watoto wao.

Baadhi ya wazazi walishindwa kujizuia na kuangua kilio baada ya kutambua miili ya watoto wao.

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu itolewe ripoti inaoonyesha zaidi ya watu 11,400 walifariki kwenye barabara za Afrika Kusini mwaka 2025, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuweka usimamizi wa mara kwa mara utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.