Wakati Simba leo Januari 20, 2026 ikimtambulisha beki kiraka Ismail Toure, timu hiyo iko mbioni kumtambulisha kiungo wake za zamani Clatous Chama kutokea Singida Black Stars ambaye inaripotiwa kwamba imeshafikia makubaliano naye.
Habari kutoka chanzo cha uhakika ndani ya Simba, imethibitisha kuwa tayari imeshafikia makubaliano na kiungo huyo na tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja.
“Chama tumeshamalizana naye na leo huenda ikawa mechi yake ya mwisho kuitumikia Singida Black Stars msimu huu. Tunataka aungane na kikosi haraka na huenda akawa sehemu ya msafara wa timu utakaoenda Tunisia kucheza na Esperance,” kimefichua chanzo hicho.
Katika mchezo wa leo, Singida Black Stars itakuwa katika Uwanja wake wa nyumbani wa KMC Complex, Dar es Salaam kukabiliana na JKT Tanzania kuanzia saa 1:00 usiku.
Kukamilika kwa usajili huo kutamfanya Chama ajiunge na Simba kwa mara ya tatu ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2018 alipojiunga akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia na mara ya pili ni 2022 alipojiunga nayo akitokea RS Berkane ya Morocco.
Katika hatua nyingine, Simba leo imemtambulisha beki Ismail Toure ambaye ni mchezaji huru aliyewahi kuitumikia Stellenbosch ya Afrika Kusini msimu uliopita.
Toure mwenye umri wa miaka 28, anamudu kucheza nafasi za beki wa kati na pia kiungo mkabaji.
Mchezaji huyo raia wa Ivory Coast anasajiliwa kuziba nafasi ya Chamou Karaboue ambaye klabu hiyo itaachana naye katika dirisha hili dogo la usajili.