Mzee Edwin Mtei Kuzikwa Januari 24 Arumeru Arusha



Mashinda Mtei, mtoto wa tatu wa aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Waziri wa zamani wa Fedha na mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), marehemu Mzee Edwin Mtei, ametangaza kuwa baba yake atazikwa Jumamosi, Januari 24, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mashinda Mtei amesema mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika katika Kata ya Ambureni, eneo la Tengeru, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambako ndipo marehemu atapumzishwa.

Mashinda ameongeza kuwa baba yake amefariki dunia Januari 20, 2026 akiwa na umri wa miaka 94, akieleza kuwa chanzo cha kifo chake ni uzee wa kawaida. Amesema katika kipindi cha takribani mwaka mmoja uliopita, afya ya marehemu ilianza kudhoofika zaidi kutokana na uzee, hali iliyomfanya kushindwa hata kuzungumza.

“Mzee alikuwa na umri mkubwa, kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita hali yake ya kiafya haikuwa nzuri kutokana na uzee, mpaka akawa hawezi hata kuzungumza,” amesema Mashinda.

Katika kipindi hiki cha maombolezo, viongozi mbalimbali wa kisiasa na watu mashuhuri wameendelea kufika nyumbani kwa marehemu kutoa pole kwa familia. Miongoni mwa waliowasili ni Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, pamoja na viongozi wengine wa chama hicho na wadau wa siasa na uchumi nchini.

Mzee Edwin Mtei anakumbukwa kama mmoja wa watu muhimu katika historia ya Tanzania, akiwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, na baadaye kuwa mwasisi wa CHADEMA, chama kikuu cha upinzani nchini.

Taifa linaendelea kuomboleza kifo cha kiongozi huyo mkongwe ambaye ameacha alama kubwa katika historia ya uchumi, siasa na demokrasia ya Tanzania.