Familia yalia na gharama za matibabu ya mtoto aliyejeruhiwa na mbwa Iringa

Iringa. Familia ya mtoto Rahmatullahi Ng’amilo (9) aliyeshambuliwa na kujeruhiwa na mbwa wazururaji katika Mtaa wa Don Bosco A, Manispaa ya Iringa imesema inaendelea kupitia kipindi kigumu cha maisha, ikikabiliwa na maumivu ya kihisia na mzigo wa gharama za matibabu.

Kwa mujibu wa wazazi wake wakizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 20, 2026 wamesema kuwa maisha ya familia yamebadilika baada ya tukio hilo, wakijikuta wakiishi kwa hofu na wasiwasi mkubwa kuhusu afya na mustakabali wa mtoto wao.

Baba wa mtoto huyo, Said Ng’amilo amesema tangu tukio hilo kutokea familia imeingia kwenye mzigo mkubwa wa kifedha kutokana na gharama za matibabu.

Ng’amilo amesema hadi sasa familia imetumia jumla ya Sh 950,000 kwa ajili ya matibabu ya mtoto wao, fedha ambazo zimekuwa juu ya uwezo wao wa kifedha.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh350,000 zilitumika kulipia huduma ya dharura hospitalini mara baada ya mtoto kufikishwa hospitali, huku Sh400,000 zikitumika kwa ajili ya huduma ya upasuaji.

“Licha ya mtoto kuwa na bima ya CHF, bima hiyo haigharamii dawa zote, hali iliyotulazimu familia kutumia Sh200,000 za ziada kununua dawa muhimu kwa ajili ya kuendelea na matibabu,” amesema Ng’amilo na kuongeza:

“Mzigo wa gharama hizo umekuwa mkubwa kwa familia, na tunalazimika kuacha shughuli za kujipatia kipato ili kumhudumia mtoto hospitalini, jambo linalozidi kudhoofisha hali ya kiuchumi,”.

Pia, Ng’amilo amesema hadi sasa familia haijapata msaada wowote kutoka serikalini, hali iliyoongeza maumivu ya gharama katika kipindi hiki kigumu.

Katika hatua nyingine Ng’amilo amesema kuwa msaada pekee walioupata umetolewa na wanamtaa wa Don Bosco A, ambao walichangisha na kutoa Sh 32,000 ili kusaidia kugharamia sehemu ya matibabu ya mtoto huyo.

Kwa sasa, familia ya mtoto huyo inaomba msaada kutoka kwa wadau na jamii kwa ujumla ili kusaidia gharama za matibabu, sambamba na kuitaka serikali na mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti kudhibiti mbwa wazururaji ili kuzuia madhara zaidi kwa watoto wengine.

Akizungumza na Mwananchi Digital Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela, amesema mtoto huyo alipokelewa Januari 8, 2026 kupitia idara ya dharura kwa ajili ya matibabu ya haraka na baada ya kupokelewa, ilibainika kuwa mbwa hao walimsababishia mtoto huyo majeraha makubwa kichwani na kwenye mapaja ya ndani, huku akiwa anatokwa na damu nyingi.

“Na mtoto huyo alihudumiwa haraka, akapatiwa chanjo ya tetenasi pamoja na chanjo ya kichaa cha mbwa ili kuzuia maambukizi hatarishi,” amesema Dk Mwakalebela.

Baada ya huduma za awali, Dk Mwakalebela amesema mtoto huyo alilazwa chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kufanyiwa upasuaji katika chumba cha upasuaji (theatre) na baadaye kuhamishiwa wodini.

Aidha kwa sasa, Dk Mwakalebela amesema mtoto huyo anaendelea na matibabu katika wodi namba 6 ya watoto, huku hali yake ikiendelea vizuri na kufuatiliwa kwa karibu na wataalamu wa afya.

Akizungumzia mwenendo wa matukio kama hayo, Dk Mwakalebela amesema hospitali hiyo hupokea kesi chache za majeruhi wa mashambulizi ya mbwa, lakini mara nyingi hupokea wagonjwa wanaogua kichaa cha mbwa na baadaye hufariki kwasababu wengi wao wakipatwa na majeraha huchelewa kwenda hospitali kupata huduma.

“Kwa mwaka jana hapa hospitali tulipokea kati ya wagonjwa 4 hadi 6 waliogundulika kuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kufariki,” amesema Dk Mwakalebela.

Rahmatullahi alipatwa na majeraha makubwa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa na mbwa wazururaji 4 mtaa wa Don Bosco A, Manispaa ya Iringa, wakati akiwa njiani kwenda shule ya msingi Nyumbatatu tukio ambalo limeibua hofu miongoni mwa wakazi na kuonesha changamoto ya kudhibiti wanyama hao katika maeneo ya makazi.