Mwanachuo afariki baada ya bodaboda aliyopanda kuigonga treni Tabora

Tabora. Mtu mmoja anayefahamika kwa majina ya Tatu Mgeta (23) amefariki dunia baada ya boda boda aliyokuwa amepanda kugonga treni ya abiria iliyokua inatoka Tabora kwenda Mpanda mkoani Katavi leo majira ya saa nne asubuhi.

Tatu alikuwa ametoka Tabora mjini kuelekea chuoni, ambapo chuo hicho kipo Ipuli hivyo wakati wanavuka barabara maeneo ya makutano ya barabara na reli eneo la Isevya, Manispaa ya Tabora dereva wa bodaboda hakuangalia umbali ilipo Treni hivyo kuigonga na kusababisha kifo cha abiria wake.

Akizungumzia tukio hilo Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Omary Simba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema dereva boda boda amepata majeraha lakini abiria wake ambaye ni mwanachuo katika Chuo cha Tabora Polytechnic aitwaye Tatu Mgeta mwenye miaka 23.

Amesema chanzo cha awali cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa bodaboda kutokuwa makini kwa sababu inafahamika kwamba kuna reli na barabara vinapishana.

“Amegharimu maisha ya binti huyu. Binti ameumia zaidi kichwani kwa sababu amerushwa kichwa kimepasuka lakini bodaboda huyu ni majeruhi amewahishwa hospitali japo hana majeraha makubwa,” amesema.

Msimamizi wa kituo cha Reli ambaye ndiye anafanya kazi ya kutoa ishara kwa watumiaji wa barabara kusubiri endapo treni inakaribia kupita, Emmanuel Matiku amesema wakati treni inakaribia amesimamisha vyombo vyote vya usafiri kusubiri ipite, lakini bodaboda huyo alipita vyombo vyote vilivyosimama akavuka ndio kuigonga treni.

“Huyu boda sijui hata alishikwa na tatizo gani kwa sababu bajaji, bodaboda wenzie walisimama hapa na hata Waterbeach kwa miguu wamesimama lakini yeye amekuja mbio kavuka na ndiyo akasababisha kifo kwa binti huyu,” amesema.

Pikipiki ambayo imegonga Treni katika eneo la makutano ya barabara na Reli eneo la Isevya manispaa ya Tabora.



Ibrahim Juma mkazi wa Kata ya Isevya Manispaa ya Tabora ambaye pia ni shuhuda wa ajali hiyo amesema uzembe wa boda kutokuzingatia sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali, imewaumiza mno.

“Yaani madereva wachache kama hawa ndio sababu ya sisi kuonekana wazembe kila siku kwa sababu ya kupuuza vitu vidogo vidogo na kusababisha madhara makubwa kwa watu wengine,” amesema.

Aidha Juma Msiri mkazi wa Manispaa ya Tabora na shuhuda wa ajali hiyo ya treni amesema boda boda kweli wana mwendo mkali wanapoendesha, lakini inachangiwa na abiria wakati mwingine wanasema tuwahi kwa sababu wana haraka na maeneo wanayokwenda.

“Kuna muda abiria anakuambia kimbiza pikipiki kwa sababu nimechelewa nataka kuwahi, kwahiyo inabidi ukimbie umridhishe abiria wako, sasa matokeo yake ndiyo ajali inatokea,” amesema.