Mwinyi awahakikishia wawekezaji vivutio vya kodi, kuondoa urasimu

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amewahakikishia wawekezaji wa ndani na nje kwamba serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kutoa vivutio vya kodi na kuondoa urasimu.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 20, 2026 wakati akizindua boti mpya ya kampuni ya Azam (Kilimanjaro IX), amesema mabadiliko makubwa ya sera, sheria na miongozo ya uwekezaji ndio yametoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendesha shughuli za biashara zenye ushindani.

“Nataka kuwahakikishia wawekezaji wa ndani na nje, serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kutoa vivutio vya kodi na kondoa urasimu na leo tunashuhudia mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali zikiwepo za baharini kampuni za kizalendo ndizo zinazoongoza kutoa huduma bora usafiri baharini,” amesema Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi amesema sekta ya usafiri baharini ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, kwani zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayotoka na kuingia nchini inapitia baharini.

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na mke Mariam, wakishuka kwenye boti ya Kilimanjaro 9 baada ya kuizindua katika bandari ya Malindi Unguja Zanzibar



Hivyo, serikali itaendelea kuimarisha sekta hiyo kuboresha bandari zote Unguja na Pemba na kuongeza bandari mpya za kisasa kutoa huduma bora za usafirishaji nchini na kupunguza msongamano katika bandari zilizopo.

Amesema kwasasa, katika ubia na sekta binafsi, serikali inaendelea na ujenzi wa bandari ya Mpigaduri ambayo itakuwa bandari ya abiria, mizigo na maegesho ya boti kwa shughuli za kitalii.

Pia, inaendelea na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani ambayo itajumuisha meli za mizigo na makasha, kupokea meli za mafuta na gesi na huduma za chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli kubwa.

Katika hatua nyingine, amesema serikali inaendelea na ujenzi wa bandari ya Fumba na zingine ili kukidhi mahitaji, “Ni matumaini yangu hatua hizi zitachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wetu kwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za abiria na mizigo nchini.”

Rais Mwinyi amesema serikali itaendelea kushirkiana na wawekezaji katika kutoa huduma za usafiri wa baharini, ili wananchi wa Zanzibar waweze kupata huduma za usafiri zenye ubora na gharama nafuu.

Ametumia hadhara hiyo, kutoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa iliyopo hivi sasa kwani Zanzibar imefunguka zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara kuweka mitaji yao hapa nchini.

Amepongeza Kampuni za Bakhresa Group, kuendelea na juhudi za kumarisha huduma za usafiri wa baharini, huku akitumia fursa hiyo pia kuwataka wazawa wengine kuiga mfano huo kuwa wazalendo na kukuza uchumi wa nchi yao.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, taarifa alizonazo, tayari kampuni hizo imeshawekeza Dola za Marekani 150 milioni wastani wa Sh381 bilioni katika sekta ya usafiri baharini na kutengeneza ajira zaidi ya 281 kwa Watanzania ikujumuisha ununuzi wa vyombo vya usafiri majini vya abiaria na mizigo vinavyotoa huduma kati ya Unguja, Pemba, Tanzania Bara na Visiwa vya Comoro.

Akitoa taarifa ya kitaalamu na hali ya uwekezaji Zanzibar, MKuregenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema kupitia sera ya uwekezaji wameendelea kusimamia na kuvutia uwekeza mkubwa katika visiwa hivyo.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano, imewekeza zaidi ya miradi 588 yenye thamani za Dola za Kimarekani 6.8 bilioni sawa na Sh17.187 trilioni, ambayo ina uwezo wa kutoa ajira 28,000.

Amesema katika mradi huo wa boti, imegharimu Dola za Marekani 12.9 milioni sawa na Sh32.624 bilioni.

Meneja wa Azam Marine, Abubakar Aziz Salum amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wamewekeza zaidi ya Sh89.7 bilioni ambapo kwa mwaka 2025 wamelipa kodi serikalini ya Sh17.5 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 18 ikilinganishwa na Sh14.9 bilioni walizolipa mwaka 2023.

Amesema uwekezaji huo umekuja kutokana na sera nzuri ya uwekezaji kisiwani humo ambapo kwa kipindi cha miaka 15, kuanzia mwaka 2010 hadi 2025, wamewekeza mtaji wa Sh300 bilioni.

Kwa mujibu wa Salum, wana meli 27 lakini ambazo zinafanya kazi zipo 10 tu zingine zimefikia mwisho wa matumizi kutokana na mazingira ya bahari.

Hata hivyo, amesema changamoto za kimazingira wanazokumbana nazo wamiliki wa meli kutokana na mkondo wa mto unaomwaga maji taka katika eneo hilo, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu vyombo hivyo na kusababisha kupiga rangi mara kwa mara.

“Tunaomba watoa huduma kushirikiana na taasisi za serikali kulinda na kuhifadhi mazingira ya bahari ili kuendelea kutoa huduma nzuri na bora kwa muda mrefu,” amesema.

Sekta binafsi imeendelea kuchangamkia fursa za usafirishaji baharini ikizingatiwa kwa takribani miaka 10 hakuna chombo chochote cha usafirishaji mizigo na abiria kinachomilikiwa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, badala yake huduma hiyo inatolewa na sekta binafsi pekee.