Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza kuanza kwa mafunzo ya kijeshi ya kujitolea kwa mwaka 2026 kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani wenye umri wa miaka 16 hadi 18.
Mkuu wa tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amezungumza hayo leo Jumanne Januari 20, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Jeshi hilo Dodoma.
“Lengo la mafunzo si kutoa ajira bali kuwaandaa vijana kukabiliana na maisha kwa kuwajengea misingi ya kujitegemea, kufanya kazi kwa nidhamu na kuchangia maendeleo ya Taifa,” amesema
Amesema mafunzo kwa washiriki yatasaidia kupata elimu ya uzalendo, nidhamu ya kazi, stadi za maisha pamoja na mafunzo ya vitendo yanayolenga kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi baada ya kuhitimu.
“Waombaji wawe raia wa Tanzania, wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 18 kwa vijana wa Tanzania Bara waliomaliza elimu ya darasa la saba na kwa vijana wa Zanzibar waliomaliza elimu ya kidato cha pili, waliomaliza masomo kuanzia mwaka 2022 hadi 2025, na kuwa na cheti halisi cha kuhitimu elimu ya msingi au kidato cha pili, “amesema.
Ametaja sifa za waombaji kujiunga na mafunzo hayo kuwa ni pamoja na vijana wenye taaluma mbalimbali hususan waliobobea katika fani za teknolojia ya habari na mawasiliano kujitokeza kuomba nafasi hizo kupitia mikoa yao.
Fani nyingine ni Stashahada ya Teknolojia ya Habari,
Stashahada ya Mifumo ya Taarifa za Biashara, Stashahada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama / ICT), Stashahada ya Usalama wa Mtandao na Stashahada ya Uchunguzi wa Uhalifu wa Kidijitali.
“Vijana wenye vipaji mbalimbali wajitokeze kwa wingi, usajili wa vijana kwa mafunzo ya JKT kwa kujitolea utaanza rasmi Januari 26, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” ameeleza.
Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana watakaoteuliwa kujiunga na mafunzo hayo watatakiwa kuripoti katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia Februari 27, 2026 hadi Machi 4, 2026.
Aidha,amewataka vijana wanaotarajia kujiunga na mafunzo hayo kufahamu kuwa jeshi hilo halitoi ajira wala halihusiki na utafutaji wa ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama, wala mashirika ya Serikali au yasiyo ya Serikali, bali hutoa mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri na kujitegemea baada ya kumaliza mkataba wao na JKT.
Amesema sifa za waombaji pamoja na maelekezo ya vifaa vinavyotakiwa kwenda navyo kuwa vinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa ambayo ni www.jkt.mil.tz.