YANGA imeondoka leo Jumatano alfajiri ikiwafuata Al Ahly ya Misri, lakini kwenye msafara wao hakutakuwa na mastaa wawili wa kigeni ambao wanandolewa rasmi.
Klabu hiyo imepanga kuwaondoa viungo Mamadou Doumbia na Celestin Ecua kwenye usajili wao ikiwa ni hesabu za kuweka sawa idadi ya wachezaji wao wa kigeni.
Awali Yanga ilikuwa na hesabu za kumuondoa kiungo, Moussa Bala Conte na Doumbia, lakini mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 yakafanya mapinduzi kweli.
Kwenye mashindano hayo, Conte akaupiga mwingi akizima kama kiungo mkabaji kisha baadaye akitumika kama beki wa kati, huku mechi ya fainali dhidi ya Azam wakati Yanga ikibeba ubingwa, alichaguliwa kuwa mchezaji bora.
Kiwango hicho kikawagawa mabosi wa Yanga ambao walianza kubishana kama wasimamie maamuzi ya awali au wabadili gia angani kutokana na kile akichoonyesha Conte.
Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves ndiye aliyeamua vita hiyo akisema Conte atabaki na badala yake Ecua atapisha nafasi.
“Ulikuwa mjadala mgumu kidogo, lakini uamuzi umefanyika Conte atabaki wakati Ecua akiungana na Doumbia kuondoka,” amesema bosi mmoja wa Yanga.
“Kocha ametusaidia sana, amefanya uamuzi wake kiufundi akaona kuna watu anaweza kuwatumia eneo ambalo Ecua alikuwa anacheza, kwa hiyo tutasimamia hapo.
“Tunataka kuwa na wachezaji ambao watashindania namba na sio mchezaji kuja kubweteka hapa kwenye klabu, uamuzi huo utawafanya wachezaji wetu kuipigania timu.”
Kwenye mchezo wa juzi ambao Yanga iliichapa Mashujaa mabao 6-0, Ecua na Doumbia hawakuonekana kikosini iwe kuanza au hata benchi, ikizidi kuleta uhakika juu ya uamuzi huo.
Yanga inafikiria kumpeleka Ecua Singida Black Stars hatua ambayo sasa itawafanya kusalia na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni baada ya kuwaongeza kiungo Allan Okello, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ na kumrudisha kwenye mfumo beki Kouassi Attohoula Yao aliyekaa nje kwa takribani miezi minane akiuguza majeraha.
Nyota 12 wa kimataifa waliobaki Yanga wanaotakiwa kikanuni ni Djigui Diarra, Kouassi Attohoula Yao, Frank Assinki, Chadrack Boka, Mousa Bala Conte, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Lasine Kouma, Allan Okello na Dilson Maria Aurélio ‘Depu’.
Ecua aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Ivory Coast alipokuwa mfungaji bora na Mchezaji Bora wa ligi hiyo kwa msimu wa 2024-2025, anaondoka Yanga akiwa amedumu kwa miezi sita akishinda mataji mawili, Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi.
Katika kipindi cha miezi sita akiwa Yanga, amefunga bao moja na asisti moja katika ligi, huku pia akipachika bao moja kwenye Kombe la Mapinduzi alipofunga dhidi ya TRA United.